Monday, June 13, 2011

WAZEE WA MSIMBAZI KATIKA PICHA YA PAMOJA



BAO pekee lililofungwa dakika ya saba na mshambuliaji Mussa Hassan 'Mgosi', liliifanya timu ya Simba kuanza vizuri kampeni yake ya kutinga hatua ya
makundi ya Kombe la Shirikisho (CAF) kwa kuifunga DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) bao 1-0.

Mchezo huo uliopigwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuhuriwa na mashabiki wachache, ulikuwa na burudani ya aina yake kwa kila timu kucheza vizuri lakini kivutio pekee kilikuwa kwa beki wa Motema Pembe, Feugang Takudjo ambaye alikuwa akirusha mipira kwa staili ya aina yake.

Katika mchezo huo, timu zote zilianza kwa kasi kwa kushambuliana kwa zamu na Motema Pembe, walionekana kutakata zaidi kwa mtindo wao wa kupiga pasi nyingi na kushambulia kwa kushtukiza.

Pamoja na hali hiyo, Simba ilipata faulo dakika ya saba baada ya Emmanuel Okwi, kufanyiwa madhambi ambapo Mgosi alikwamisha mpira wavuni kutokana na mpira uliopigwa na Mohamed Banka, aliyeunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Okwi.

Baada ya kufungwa bao hilo, Motema Pembe iliendelea kutawala mchezo na dakika ya 17, Ilongo Ngasanya alishindwa kukwamisha mpira wavuni kutokana na mpira uliorushwa na Takudjo, kuwachanganya mabeki wa Simba.

Beki Takudjo alikuwa kivutio kwa kuwa kabla ya kurusha mpira alilazima kubinuka sakarasi, kitendo kilichowachanganya waamuzi na kufikia wakati kujadiliana juu ya mtindo huo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikionekana kutafuta bao, lakini dakika ya 63, Bokota Labama wa Motema nusura aisawazishie timu yake bao lakini alishindwa kuunganisha krosi iliyopigwa na Salakiaku Matonda.

Motema ilizidisha presha kwa Simba na dakika mbili baada ya tukio hilo, beki Haruna Shamte wa Simba alioneshwa kadi ya pili ya njano na baadaye nyekundu na mwamuzi Solomon Wakoma, kutoka Nigeria na kutoka nje kwa kumchezea vibaya Matonda.

Wakati mchezo ukiendelea, dakika ya 68 mwamuzi Wakoma alijichanganya baada ya kupuliza filimbi ya kuotea kwa wachezaji wa Motema.

Simba ilijaribu kutuliza mashambulizi ya wapinzani wao kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwa kutumia mipira mirefu, lakini haikuzaa matunda kwani mabeki wa Motema walikuwa makini kuondosha hatari hizo.

Zikiwa zimebaki dakika mbili kabla ya filimbi ya mwisho kupulizwa, Diavita Dama aliyeingia badala ya Landu Makela alikosa bao la wazi kwa kushindwa kuunganisha krosi ya Ilongo.

Simba: Juma Kaseja, Shamte, Amir Maftah, Juma Nyosso, Yondani, Amri Kiemba, Nicco Nyagawa, Juma Jabu, Okwi, Mgosi/Salum Kanoni na Banka.

No comments:

Post a Comment