Saturday, June 18, 2011

Jaji Mkuu Othman Chande (kushoto) akionesha vitabu vya haki na utii bila shuruti baada ya kuzindua kampeni ya kuhamasisha jamii kuhusu utii wa sheria bila shuruti katika Bwalo la Maofisa wa Polisi Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi , Said Mwema.

HABARI ZAIDI

VIONGOZI wa siasa nchini wametakiwa kupanda mbegu za maadili mema kwa wafuasi wao, huku wao wenyewe wakionesha mfano wa kuwa mstari wa mbele kutii sheria za nchi.

Aidha, wametakiwa kuelewa, kwamba tafsiri ya kupenda nchi si kufanya harakati za kuchochea ukiukwaji wa sheria.

Hayo yalisemwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, katika hotuba yake ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha jamii kuhusu utii wa sheria bila shuruti uliofanyika kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Alisema uzinduzi wa kampeni hizo umekuja kwa wakati mwafaka, hasa katika kipindi ambacho nchi imekumbwa na matukio ya wananchi kujifanya wanadai haki, lakini bila kuzingatia wajibu walionao kisheria.

Katika hotuba yake, aliyoitoa mbele ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwamo makamanda wa Polisi wa mikoa yote nchini, wawakilishi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wa asasi za kiraia, alisisitiza juu ya utekelezaji wa kampeni hiyo kwa vitendo, kwa kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Jaji Mkuu pia aliwataka viongozi wa dini kuelewa kwamba wana wajibu mkubwa wa kuongoza dhamira za wafuasi wao kutenda mema, kuhimiza na kulinda maadili ya jamii kwa ajili ya kujenga amani na umoja wa kitaifa.

Kwa upande wa asasi za kiraia, alisema nazo zina jukumu kubwa kwa umma wa Watanzania wanaopaswa kupewa elimu chanya ya uraia na uzalendo, huku wakitimiza maadili mema ya kitanzania.

Akimkaribisha Jaji Mkuu kuzindua kampeni hiyo, IGP Mwema alisema kampeni hiyo itakayosambaa hadi ngazi za mashina, inalenga kuwaamsha na kuwapa hamasa Watanzania kuirejea misingi ya uwajibikaji katika harakati za kudumisha amani, usalama na utulivu, kama mtaji wa kujiletea maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii nchini.

No comments:

Post a Comment