ZAIDI ya Shilingi 73,000,000 zimekusanywa na mamlaka ya hifadhi ya taifa TANAPA katika kipindi cha Oktoba mwaka jana hadi Mei mwaka huu kufuatia malipo ya adhabu ya wafugaji kuingiza mifugo katika hifadhi ya Ruaha upande wa eneo la Ihefu wilayani Mbarali.
Kwa mujibu wa kaimu mhifadhi mkuu wa hifadhi ya Ruaha Dodwell Ole Meing’ataki baadhi ya wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo hususani ng;ombe katika maeneo ya hifadhi jambo ambalo ni kinyume na sheria hivyo TANAPA kulazimika kuwawajibisha wanapowakamata.
Meing’ataki alisema mwezi oktoba mwaka jana mamlaka ilikusanya kiasi cha shilingi milioni moja na mwezi disemba milioni 19, lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda mifugo zaidi ikaendelea kuingizwa ndani ya hifadhi.
Alisema mnamo Januari mwaka huu Tanapa ilikamataa mifugo 500 na kutoza faini ya jumla ya shilingi milioni 12,April wakakamataa mifugo 1600 na kutoza zaidi ya shilingi milioni 30 na mei ikakamatwa mifugo 700 ambapo zilipatikana milioni 11.
Kaimu mhifadhi mkuu huyo alisema makundi ya mifugo yamekuwa yakiingizwa hifadhini nyakati za usiku ambapo ni vigumu kufanya doria kwa kutumia helkopta na inapofika asubuhi mifugo hiyo hurejeshwa katika maboma ya wafugaji.
Hata hivyo alifafanua kuwa tatizo la wafugaji kuingiza mifugo yao ndani ya hifadhi linaonekana kusababishwa na makundi makubwa ya mifugo inayoonezeka katika vijiji vinavyozunguka hifadhi ambapo inasadikiwa wafugaji waliohamishwa kupisha hifadhi wanarejea katika vijiji hivyo.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa John Mwakipesile aliipongeza TANAPA kwa kutoza faini kwa wafugaji wakaorofi akisema kazi hiyo ni kubwa na pasipo kufanya hivyo wafugaji wangesababisha kupotea kabisa kwa eneo oevu la Ihefu lililo chanzo kikubwa cha maji yam to Ruaha yaliyotegemeo katika bwawa la kuzalisha nishati ya umeme la Mtera.
Mwakipesile alisisitiza mamlaka nyingine zilizo karibu na hifadhi hiyo kuona haja ya kusaidia mikakati ya TANAPA katika kulinda hifadhi hiyo huku akiutaka uongozi wa serikali ya wilaya ya Mbarali kuwachukulia hatua viongozi wa vijiji wanaopokea wafugaji waliohamishwa kutokana na kuwa na makundi makubwa ya mifugo.
No comments:
Post a Comment