Friday, July 29, 2011

JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA KUENDELEA KUFANYA UCHUNGUZI WA MGOGORO

JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA KUENDELEA KUFANYA UCHUNGUZI WA MGOGORO
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Mbeya ADVOCATE NYOMBI amesema jeshi lake linaendea na uchunguzi ili kubaini ukweli wa mgogoro kati ya wananchi wa kijiji cha kapunga wilayani Mbarali mkoani Mbeya dhidi ya mwekezaji wa kampuni Rice Project

Kuhusu vitendo vya uharibifu wa mali za wananchi Kamanda NYOMBI amesema hana taarifa nazo na kwamba na kuwataka wananchi hao kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea.

Hata hivyo habari tulizozipata zinadai kuwa mwekezaji huyo alivunja matofali kumi na mbili elfu ambayo yalifyatuliwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi Mbarali na kumjeruhi mwanakijiji kwa kumgonga na gari.
 
MAITI YA MTOTO MCHANGA YATUPWA JALALANI MBEYA.
Maiti ya mtoto mchanga imekutwa ndani ya mfuko wa Rambo uliotupwa kwenye dampo la shule ya msingi ya Sinde liliyopo kata ya Ruanda mtaa mtoni jijini Mbeya.

Habari za kukutwa kwa maiti ya mtoto mchanga zimetolewa na watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi ambao walikuwa wanaokota mifuko hiyo kwenye dampo hilo kwa ajili ya kwenda kuziuza kwa wafanyabiashara wa mkaa.

Imeeleza kuwa baada ya watoto hao kuifungua Rambo ndipo walipokutana na maiti ya mtoto mchanga na kutoa taarifa kwa wafanyabiashara na wakazi wa mtaa wa Mtoni ambao nao walitoa taarifa kwa jeshi la polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Hata hivyo hakuna mtu anayehisiwa kwenye mtaa huo kuhusika na tukio la kutupwa kwa maiti hiyo, Jeshi la polisi lilifika eneo hilo majira ya saa mbili za usiku na kuondoka na mwili wa mtoto huyo ambaye anadaiwa kuwa na siku moja tangu azaliwe.

UKOSEFU WA VITENDEA KAZI KITUO CHA AFYA NSONYANGA - MBARALI
Kituo cha afya cha Nsonyanga kilichopo kijiji cha Kapyo kata ya mahongole wilayani mbarali mkoani Mbeya kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vitendea kazi, usafiri kwa ajili ya wagonjwa, nyumba za watumishi na upatikanaji wa nishati ya umeme.

Mkuu wa kituo hicho Dakta EDSON MWANDEUKA amesema wanalazimika kutumia taa ya Chemli wakati wa kutoa huduma za uzazi kwa wakina mama wajawazito nyakati za usiku hali inayohatarisha usalama wa afya kwa wakina mama hao.
Kutokana na tatizo hilo mwenyekiti wa kijiji hicho bwana KYANDO amesema uongozi wa kijiji chake unaendelea na mchakato wa kufanikisha kituo hicho kinapata nishati ya Umeme ili kurahisisha zoezi la utoaji wa huduma kwa wagonjwa nyakati za usiku.

Kituo cha Nsonyanga kina wauguzi 3 ambapo kituo hicho kinahudumia vijiji vya kapyo, uswisi, ilongo, Nsonyanga, azimio mapula, malawato na mkoi.

MAONYESHO YA KILIMO MWAKA HUU MKOANI MBEYA YAVUNJA REKODI.
Maonesho ya Kilimo ya mwaka huu yamevunja rekodi ya mwaka jana baada ya kujitokeza wadau wapatao 400 watakaoshiriki kwenye maonesho hayo ikilinganishwa na ya mwaka jana ambayo wadau takriban 300 ndio walioshiriki maonesho hayo.

Kwa upande wa miundo mbinu KASILATI amesema TASO imejiandaa kuhakikisha barabara zinachongwa vizuri, huduma za Afya zinatolewa uwanjani humo, maji yanapatikana licha ya changamoto ya nishati ya Umeme kuwepo.

Aidha Bwana KASILATI ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo yatakayoanza rasmi tarehe moja mwezi wa Nane.

UZOAJI TAKATAKA WAENDELEWA KUSUASUA MJI MDOGO WA MBALIZI MBEYA VIJIJINI.
Wafanyabiashara wa soko la Tarafani Mbalizi Wilaya ya Mbeya vijijini wameulalamikia uongozi wa soko hilo kwa kushindwa kutoa takataka zilizojaa kwenye Dampo la soko hilo kwa mda mrefu.

Wamesema halmashauri ya wilaya hiyo haina utaratibu wa kuzoa na kutupata taka pindi zinapo jaa kwenye dampo hali inayopelekea kuwepo kwa harufu mbaya sokoni hapo.

Mmoja wa wafanyabishara wa soko hilo RASHIND EFRAIMU amesema wamekuwa wakilipia ushuru kila siku na kwamba kinachowakera ni kuona takataka zikiendelea kurundikana kwenye dampo ikiwa ni pamoja na miundombinu ya soko kuendelea kuwa mibovu.

Nao wauzaji wa chakula wameuomba uongozi wa halmashauri ya Mbeya Vijijini kuchukuwa hatua za haraka za kuondoa taka kwenye madampo ili kuondoa kero ya harufu mbaya inayopelekea kukimbiwa na wateja.

Afisa afya wa soko hilo MHEMEJI amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa uchache wa magari ya kubebea taka ndio sababu ya kusuasua kwa zoezi la uzoaji wa taka.

Kwa hisani ya CHIMBUKO LETU Blogu http://ukurasampyahuu.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment