Saturday, July 23, 2011

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA MHESHIMIWA BERNAD MEMBE (MB)AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012

                                   WAZIRI MHE. BERNARD KAMILLIUS MEMBE
A. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

2. Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nachukua fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne. Pili, ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kunichagua kwa mara nyingine tena kuongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Aidha, ninampongeza Dkt. Mohammed Gharib Bilal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, ninampongeza Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, (Mb.) kwa kuchaguliwa bila kupingwa kuwa Mbunge na kuteuliwa tena na Mhe. Rais na hatimaye kuthibitishwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Waziri Mkuu kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne.

3. Mheshimiwa Spika, napenda nikupongeze kwa kuchaguliwa kwa kishindo kushika nafasi ya Spika wa Bunge letu tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu, miaka 50 iliyopita. Uteuzi wako ni kielelezo cha ukomavu wa demokrasia ya nchi yetu na imani kubwa tuliyonayo sisi Waheshimiwa Wabunge, juu ya utendaji wako uliotukuka. Kadhalika, nampongeza Naibu Spika, Mhe. Job Ndugai pamoja na Wenyeviti kwa kuchaguliwa katika kusaidia uendeshaji wa Bunge hili tukufu. Napenda pia kuwapongeza Mawaziri wenzangu pamoja na Naibu Mawaziri wote, kwa kuteuliwa kwao na Mhe. Rais kushika nyadhifa hizo. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupata heshima na dhamana kubwa ya kuwawakilisha wananchi wa majimbo pamoja na makundi mbalimbali ya jamii katika Bunge hili.
4. Mheshimiwa Spika, naomba kwa namna ya pekee niwashukuru Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) na Waziri wa Fedha, Mhe. Mustafa Haidi Mkulo (Mb.) kwa hotuba zao ambazo zimetoa mwelekeo wa Taifa letu katika mwaka huu wa fedha. Hotuba zao zimegusia mambo ya kimsingi yanayohusu Wizara yangu. Naomba pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Mawaziri wenzangu wote walionitangulia katika kuwasilisha hotuba zao kwa kuzungumzia kwa ufasaha baadhi ya masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa wanayoyashughulikia katika Wizara zao. Wizara yangu imekuwa ikishirikiana vyema na kwa karibu sana na Wizara hizi, na mara zote imekuwa ikizingatia ushauri wao kwa umakini mkubwa.

5. Mheshimiwa Spika, napenda pia niwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya Uenyekiti wa Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.) kwa ushauri wao ambao umekuwa wa msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu ya Wizara yangu kwa mafanikio.

6. Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye ameendelea kuwa wa msaada mkubwa kwangu katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Aidha, namshukuru Katibu Mkuu, Bwana John M. Haule; Naibu Katibu Mkuu, Balozi Rajabu Gamaha, Wakurugenzi wote, Mabalozi wetu pamoja na wafanyakazi wenzangu wote Wizarani na katika Balozi zetu kwa bidii na kujituma kwao ipasavyo katika kutetea na kulinda maslahi ya nchi yetu ndani na nje na pia kwa kufanikisha kwa wakati hotuba hii ya bajeti.

7. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wapiga kura wangu na wananchi wa Jimbo la Mtama, kwa upendo wao na imani yao kwangu. Napenda pia niwashukuru viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wa Mkoa wa Lindi kwa uongozi thabiti na kwa ushirikiano wao mkubwa. Kwa upande wa familia yangu, ningependa kumshukuru sana mke wangu, Dorcas Membe, pamoja na watoto wetu kwa kunitia moyo na nguvu katika shughuli zangu za kila siku. Mama Membe hayupo pale juu leo kwa sababu yupo nje ya nchi akimuuguza kijana wetu Denis ambaye amefanyiwa upasuaji mkubwa na namtakia afya njema.




B. HALI YA DUNIA NA CHANGAMOTO ZILIZOPO

8. Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi na usalama duniani kwa ujumla ni shwari isipokuwa katika maeneo machache ambayo yanahitaji uangalizi wa makini wa jumuiya ya kimataifa.

9. Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi katika nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, imeendelea kuimarika baada ya kipindi kigumu cha mdororo wa uchumi uliyoikumba dunia mwaka 2008 licha ya baadhi ya nchi kama Ugiriki, Uhispania na Ureno kuendelea kusuasua katika kuimarisha uchumi wao. Kwa ujumla, hali ya usalama duniani inatia moyo ingawa kuna maeneo machache ambayo yamegubikwa na migogoro ya ndani, iliyosababishwa na shinikizo la kutaka mabadiliko ya kisiasa, kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa ajira. Hali hiyo imeleta madhara makubwa katika nchi ambazo hazikuingia katika mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaliyoanza katika miaka ya themanini hadi miaka ya tisini. Madhara hayo ni pamoja na vifo vya raia, ongezeko la wakimbizi, uharibifu wa miundombinu, kuzorota kwa shughuli za uzalishaji na hivyo kuongezeka kwa umaskini na hatari ya kuibuka kwa vitendo vipya vya kigaidi. Wizara yangu imeendelea kufuatilia na kushiriki kikamilifu katika michakato ya kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro hiyo.

No comments:

Post a Comment