TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Julai 20, 2011, ametumia siku ya pili ya ziara yake ya kihistoria katika Afrika Kusini kwa kutembelea na kushawishi wawekezaji wa kilimo cha zabibu na utengenezaji divai kutoka nchi hiyo kuwekeza katika kilimo cha zao hilo mkoani Dodoma.
Aidha, Rais Kikwete ametembelea Kisiwa cha Robben, kilichoko kilomita 12 kutoka mjini Cape Town ambako viongozi wakuu wa mapambano ya kupinga siasa za ubaguzi wa rangi za makaburu walifungwa kwa vipindi kirefu wakiwemo marais watatu kati ya wanne walioongozwa Afrika Kusini tokea Uchaguzi Mkuu wa Kidemokrasia wa mwaka 1994 – Waheshimiwa Nelson Mandela, Kgalema Mothlante na Jacob Zuma.
Rais mwingine ambaye ameongoza Afrika Kusini tokea wakati huo, Mheshimiwa Thabo Mbeki hakufungwa katika Kisiwa hicho lakini baba yake hayati Govin Mbeki alifungwa na akina Mandela kwenye Kisiwa hicho.
Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete na ujumbe wake ametumia siku ya pili ya ziara yake ya kidola katika Afrika Kusini kutembelea mashamba ya zabibu na kiwanda cha kutengeneza divai katika Jimbo la Cape Magharibi ambalo mji wake mkuu ni Cape Town.
Rais Kikwete amewasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cape Town asubuhi ya leo akitokea Pretoria na kwenda moja kwa moja kutembelea Kisiwa cha Robben ambako alitembezwa kwa kiasi cha dakika 40 kabla ya kuelekea kwenye shamba na kiwanda cha kupanda zabibu na kutengeneza divai la Waterford Estate lililoko katika eneo la StellenBosch, eneo maarufu kwa zao la zabibu na utengenezaji wa divai.
Akizungumza na wenye kiwanda cha Waterford, Rais Kikwete amewaomba kufikiria kwa makini uwezekano wa kuwekeza katika mashamba ya zabibu na utengenezaji divai kwa kushirikiana na wakulima wadogo wadogo wa eneo la Dodoma.
“Naomba mfikirie kwa makini kabisa ombi langu la kuwataka mje kuwekeza katika kilimo cha zabibu na utengenezaji divai kwa kushirikiana na wakulima wa Mkoa wa Dodoma. Katika mkoa huu, zabibu huvumwa mara mbili kwa mwaka tofauti na nchi nyingine duniani na wakulima katika eneo hilo wanaweza kunufaika na ujuzi na uzoefu wenu na kuwapandia zabibu kwa ajili ya kuendesha kiwanda chenu,” Rais Kikwete amewaambia wakulima hao.
Kiwanda cha Waterford kilianzishwa Aprili mwaka 1998 na familia mbili ambazo ni ile ya Jeremy na mke wake Leigh Ord pamoja na ile ya Kevin Arnold ambaye ni mtengenezaji divai pamoja na mkewe.
Kiwanda hicho ambacho kwa sasa kinatengeneza kiasi cha masanduku 35,000 ya divai kwa mwaka ikiwa ni divai nyekundu na nyeupe ni moja ya viwanda vinavyoongoza katika Afrika Kusini kwa kutengeneza divai bora duniani.
(Att. Media: Kurugenzi ya Mawasiliano leo, Alhamisi, Julai 22, itatoa Makala Maalum kuhusu ziara ya Mheshimiwa Rais Kikwete katika Kisiwa cha Robben).
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Pretoria
Afrika Kusini.
22 Julai, 2011
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesisitiza, kwa mara nyingine tena, kuwa Serikali yake haijapata kukusudia wala haina mipango ya kujenga barabara ya lami kukatisha katikati ya mbuga maarufu duniani ya Serengeti iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kama yupo kiongozi ambaye amethibitisha wakati wote wa uongozi wake kuwa mtetezi mkubwa wa mazingira na kulinda mbuga za wanyama basi ni yeye mwenyewe.
“Serengeti ni tunu ya taifa letu. Kamwe hatuwezi kuchukua hatua zozote za kuharibu ama hata kuvuruga hali ya Serengeti. Ni tunu ya Tanzania, ina thamani kiuchumi kwa wananchi wetu na kwa nchi yetu na ni moja ya maeneo machache duniani ambayo dunia inayatambua kwa upekee na umuhimu wake na inayalinda,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema hayo juzi, Jumanne, Julai 19, 2011 wakati anamjulisha Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Zuma na mawaziri wa Baraza la Mawaziri la kiongozi huyo wa Afrika Kusini kuhusu mkanganyiko ambao umezuka, kwa bahati mbaya sana duniani, kuhusu mipango ya Serikali ya Rais Kikwete kuwapatia wananchi wanaoishi Kaskazini mwa Mbuga ya Serengenti barabara ya uhakika ili kumaliza matatizo yao makubwa ya maendeleo.
Rais Kikwete alitoa maelezo hayo kwa viongozi hao wa Afrika Kusini wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Serikali za Tanzania na Afrika Kusini kwenye Majengo ya Muungano (Union Buildings) mjini Pretoria, Afrika Kusini.
Mazungumzo hayo yalikuwa moja ya shughuli za mwanzo kati ya shughuli nyingi za Mheshimiwa Rais Kikwete wakati wa ziara yake ya kidola ya kihistoria ya siku tatu katika Afrika Kusini iliyomalizika jioni ya leo, Jumatano, Julai 20, 2011. Rais Kikwete anaondoka Afrika Kusini kurejea nyumbani kesho, Alhamisi, Julai 21, 2011.
Rais Kikwete alimwambia Rais Zuma na mawaziri wake kuwa umekuwepo mchanganyiko usiokuwa wa lazima kabisa kuhusu mipango ya Serikali kuwapatia barabara wananchi wa maeneo yasiyofikika kwa urahisi kati ya Mto wa Mbu, mkoani Arusha hadi Makutano, mkoani Mara kupitia Loliondo, Mugumu na Nata.
“Nataka kuzungumzia kidogo suala la madai kuwa Tanzania inataka kujenga barabara ya lami kukatisha Mbuga ya Wanyama ya Serengeti. Sijui mkanganyiko kuhusu suala hili umetoka wapi lakini ukweli ni kwamba Serikali ya Tanzania haikusudii na wala haina mipango ya kujenga barabara ya lami kupitia mbuga hii muhimu sana kwa Tanzania na kwa dunia nzima.”
“Tunachosema ni kwamba Serikali yetu inao wajibu wa aina mbili. Kwanza ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanaoishi Kaskazini mwa Serengeti wanapatiwa barabara ya uhakika ili kusaidia kufungua fursa zao za maendeleo.
Hawawezi kuendelea kufanywa kama sehemu ya utalii kwa kubakia katika hali ya udhalili. Pili ni kuhakikisha kuwa tunalinda Mbuga la Serengeti kama ambavyo tumefanya miaka yote tokea uhuru wetu mwaka 1961.”
“ Mipango yetu ni kuhakikisha kuwa sehemu nzima ya barabara inayokatisha Mbuga hiyo inabakia bila lami na wala siyo kweli kuwa tunalenga kuharibu Mbuga hiyo. Sisi ndio watunzaji wakuu wa mbuga hii na mbuga zote za wanyama za Tanzania, inakuwaje leo sisi ndiyo tunaambiwa kuwa tunakusudia kuharibu mbuga hizo? Binafsi tokea kuchukua nafasi ya Urais wa Tanzania mapumziko yangu yamekuwa katika mbuga zetu za wanyama…hata juzi, siku nne kabla ya kuja hapa nilikuwa Serengeti.”
Aliongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Ni jambo la kusikitisha sana kuwa wapo watu ambao wanapinga ujenzi wa barabara hii ambayo wala haitakatisha kwa lami katikati ya mbuga hiyo. Wanasahau kuwa hawa watu tunaotaka kuwajengea barabara waliondolewa katika Mbuga hiyo ambamo walikuwa wanaishi. Waliondoka bila matatizo yoyote sasa kwa nini Serikali isiwajibike kwa kuwapatia nyenzo muhimu ya maendeleo kama barabara.”
Baada ya maelezo hayo, Rais Zuma alimwambia Rais Kikwete: “Tunaunga mkono moja kwa moja msimamo wa Tanzania kuhusu suala hili. Tunaelewa tatizo ambalo Serikali yako, Mheshimiwa Rais, inajaribu kulitatua la kuleta maendeleo kwa wananchi wake.”
Barabara ya Mto wa Mbu-Loliondo-Mugumu-Nata-Makutano yenye kilomita 452 ni miongoni mwa barabara zenye jumla ya kilomita 11,000 ambazo Serikali ya Rais Kikwete anazijenga ama kuanza kuzijenga katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake. Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ujenzi wa barabara hiyo unatakiwa kuanza katika kipindi cha sasa.
Akizungumza baadaye usiku katika dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais Zuma kwa ajili yake kwenye Nyumba ya Urais ya Afrika Kusini, Rais Kikwete aliisifu Serikali ya Afrika Kusini kwa kuonyesha uongozi katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili Bara la Afrika.
“Mheshimiwa Rais tulishughulikia kwa pamoja matatizo ya Burundi na sasa nchi hiyo imetulia. Umeshughulikia suala la Zimbabwe ambalo bado linahitaji jitihada zako. Kwa pamoja tulihangaika na Ivory Coast na tunawatakia heri waanze kuijenga upya nchi hiyo na sasa una changamoto ya Libya. Napenda kukupongeza kwa mchango wako katika kuleta utulivu na amani katika Bara letu.”
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Pretoria
Afrika Kusini.
22 Julai, 2011