Thursday, August 11, 2011

YALIYOJILI MKOANI MBEYA NA MBN BLOGU KATIKA KUENDELEZA TAIFA

MIUNDOMBINU MIBOVU NI CHANZO CHA KUSUASUA
Ubovu wa miundombinu ya barabara katika wilaya ya Ileje mkoani Mbeya imetanjwa ndio sababu kuu inayoleta usumbufu kusafirisha pembejeo za ruzuku ikiwemo mbolea hizo wakati wa masika

Kwa upande wake Afisa ushauri wa kilimo wilayani humo bwana Labron Kibona alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuitupia lawama wizara ya kilimo chakula na ushirika kuwa wanachelewa kutoa hela za vocha.

Wakati huo huo Wakulima wa Tarafa ya Bundali Wilayani Ileje wameilalamikia serikali kwa kitendo cha kuwacheleweshea mbolea ya ruzuku kwa madai ya kwamba wakulima hao wanategemea kilio cha mvua kitu ambacho sio cha kweli.

Akizungumza nasi mmoja wa wakulima hao kutoka kijiji cha Isongole Bwana Nickson Sengo alisema kutokana na mvua kutokuwa ya uhakika watu wengi wilayani humo wanategemea zaidi kilimo cha umwagiliaji ambacho huanza mwezi wa tisa.

Aidha Sengo anaiomba serikali kuwahisha mbolea kabla mvua hazijaanza kunyesha kufuatana na kwamba barabara nyingi katika maeneo hayo zinapitika kiangazi.

----------------
MCHUNGAJI MWALEGA AKEMEA VIKALI WIZI UNAOFANYWA NA BAADHI YA WAUMINI
Mchungaji wa KKKT Jimbo la Mbeya Dayosisi ya Konde Nazareti Mwalwega amekemea vikali wizi unaofanywa na baadhi ya waumini kwa kutomtolea MUNGU sadaka zipasazo kulingana na mapato yao.

Akihubiri katika usharika wa Iwambi ambapo Mkuu wa Jimbo la Mbeya Mchungaji Andindilile Mwakibutu akiwa katika sherehe za kumsimika Mchungaji Mmenye Mwasampeta kwa kazi za usharikani hapo amesoma kitabu cha Mithali 3:9-10 na Malaki 3:9-10 na kusisitiza kwamba kulingana na Biblia kutomtolea MUNGU sadaka ni wizi.

Mwalenga alisema kuwa kutomtolea MUNGU sadaka kama vile zaka malimbuko shukrani ni dhambi na kumtolea ni baraka kwani MUNGU humzidishia kila amtoleaye kwa moyo.

Katika kuwaandaa waumini wa usharika wa Iwambi ambao watakuwa na sikukuu ya mavuno tarehe 21 mwezi huu Mwalwega alisisitiza kila mmoja kutoa sadaka kwa moyo kulingana na uwezo wake wa hali na mali.

Pia alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waumini juu ya umuhimu wa kuwasaidia yatima wagonjwa na wenye matatizo mbalimbali bila kujali tofauli zao vilevile ibada hiyo iliyofurika watu ilipambwa na kwaya ya Jimbo kwaya kutoka usharika wa Tunduma na kwaya ya wenyeji.

-----------------
WANANCHI MKOANI MBEYA WAISHUKURU BOT.
Wakazi wa mkoa wa Mbeya wameishukuru benki kuu ya Tanzania (BOT) kwa elimu waliyoitoa juu ya kuzitambua fedha bandia.

Wakiongea nasi baadhi ya wananchi wamesema mara nyingi wamekuwa wakipokea fedha hizo pasipo wao kujua jambo ambalo linawaletea usumbufu mkubwa hasa katika maendeleo ya kiuchumi.

Naye mmoja wa wafanyabiashara wilayani Ileje Bi.Agnes Sokwa aliwaomba wananchi kuwa makini katika suala hilo na kutowafumbia macho wale wote watakaobainika kujihusisha na usambazaji wa fedha hizo.

Aidha wakazi hao wameziomba taasisi nyingine za fedha Tanzania kushirikiana na serikali katika kutoa elimu hiyo maeneo yote na muda wote ili kuhakikisha thamani ya fedha ya Tanzania inatunzwa na kuheshimiwa.

Hata hivyo hivi karibuni yalilipotiwa baadhi ya maeneo yanayoongozwa kwa upatikanaji wa pesa bandia mkoani Mbeya kuwa ni Eso, Soweto, Iyunga na Mafiati ambapo changamoto zilikuwa zikiwakabili madereva bodaboda wakati wa upokeaji wa nauli kutoka kwa abiria zao hali iliyokuwa ikichangia kupata hasara mara baada ya kurudisha chenji.

TUREJEA MSIMU WA NANENANE- WANANCHI WAPEWE ELIMU KUHUSU TTCL

Wananchi wanatakiwa kupewa elimu juu ya umuhimu wa shirika la mawasiliano Tanzania (TTCL) na huduma zake ili waweze kuzitumia kwa ufasaha.

Akizungumza mmoja wa wafanyakazi wa TTCL katika uwanja wa maonyesho nanenane jijini Mbeya bwana Amos Humbo alisema wananchi wengi wanashindwa kutumia huduma za shirika hilo kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya huduma zao.

Aliongeza kuwa huduma ya simu za mkononi haziwafikii wananchi wote kutokana na uchanga wa huduma hiyo na gharama ya minara ya mawasiliao katika shirika hilo ikizingatiwa kwamba halitegemei ruzuku kutoka serikalini.

Aidha bwana Humbo aliiomba serikali kulisaidia shirika hilo ili kuweza kufanikisha malengo yake ya kuwafikia wananchi wote na kwa gharama nafuu ili kila mwananchi aweze kunufaika na huduma hizo.



Tuesday, August 9, 2011

HUKU NA KULE MKOANI MBEYA

VIJIJI VITATU WILAYANI ILEJE VYA NUFAIKA NA HUDUMA YA MAJI MASAFI
Vijiji vitatu wilayani Ileje mkoani Mbeya vimeanza kufaidika na huduma ya maji safi yatokanayo na visima.

Hayo yamesemwa na afisa mipango wa wilaya hiyo Bwana Lawlent Swila katika mkutano wa maendeleo uliowahusisha walimu wakuu, madiwani, wanafunzi wote wa vyuo vikuu na wadau wengine wa maendeleo wilayani humo.

Amevitaja vijiji vilivyonufaika kuwa ni Isoko, Mbebe na chembe ambavyo vimejengewa visima virefu mita 90 ambapo kijiji cha Isoko kimefungwa bomba za kupitisha maji safi.

Naye diwani wa kata ya Bupigu Ubatizo Songa ametoa pongezi kwa Serikali wilayani humo katika kuwafikishia wananchi wake huduma muhimu ya maji na kuwataka viongozi wenzake kushirikiana kikamilifu kuilinda miradi hiyo isiharibiwe.

CHUO KIKUU CHA KILIMO SOKOINE KIMETOA ELIMU KWA JAMII UMUHIMU WA CHAKULA

Chuo kikuu cha kilimo Sokoine kimetoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chakula kwa binadamu katika maadhimisho ya maonesho ya kilimo nane nane mkoani Mbeya.

Mkuu wa chuo hicho profesa Joyce Kinabo amesema jamii inatakiwa kujua umuhimu wa vyakula mbalimbali katika kujenga miili yao.

Wakati huohuo ameitaka jamii kunywa maji mara pamoja na matunda kwani kwa kufanya hivyo kutasawasaidia kujenga afya zao.


WAZIRI DAVID MATAHAYO ATOA PONGEZI KWA MKUU WA MKOA WA MBEYA BWANA MWAKIPESILE
Waziri wa mifugo na Biashara David Mathayo ametoa pongezi kwa mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakangale kwa juhudi alizozionesha kutokomeza ugonjwa wa mafua ya Nguruwe.

Amesema hayo wakati akifunga maonesho ya kilimo nane nane Ambayo yamefanyika kikanda mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale vilivyopo kata ya Uyole jijini hapa.

Aidha ametoa pongezi kwa viongozi wa mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini kwa kusimamia na kutekeleza vyema Sera ya kilimo kwanza kwa kufanikiwa kuzalisha mazao mengi ambapo mikoa hiyo Mbeya, Iringa Rukwa na Ruvuma imefanikiwa kuzalisha zaidi ya Tani milioni 5 za chakula kwa msimu huu wa kilimo ambazo zitasaidia kupunguza tatizo la njaa hapa nchini.

Wakati huohuo Waziri Mathayo amemtunuku mshindi wa kanda katika maonesho hayo Dickson Sengo mkulima wa kata ya Isongole wilayani Ileje mkoani Mbeya power Tiller moja na Cheti cha Ushindi.

Kwa hisani ya CHIMBUKO LETU 

Saturday, August 6, 2011

SHILINGI MIL 52 ZIMETOLEWA KUTUMIKA KIPINDI CHOTE CHA MAONESHO YA NANENANE MKOANI MBEYA

Zaidi ya shilingi milioni 52 zimetolewa kutumika katika kipindi chote cha maonesho ya kilimo Nanenane yanayoendelea kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile amesema fedha hizo ni kwaajili ya shughuli za maonesho ili yafanywe na ya vutie miongoni mwajamii.

Aidha ameitaka kamati ya kusimamia maonyesho hayo kuakikisha fedha zilizopatikana zinatumika kama ilivyo kusudiwa na kuwataka wamiliki wa wa vibanda vilivyopo nje ya uwanja huo kuvikamilisha ili kuondokana na hatari ya kufutiwa usajili wa maeneo yao.
HABARI ZA HUKU NA KULE.
WALEMAVU WAVVU NCHINI TANZANIA WASHAURIWA WASIKATE TAMAA

Watu wenye ulemavu na wale wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi wameshauriwa kutokata tamaa ya maisha pindi wanapakabiliana na changamtoto mbalimbali ndani ya jamii.

Ushauri huo umetolewa na mkuu wa kikundi cha jipe moyo bwana Kaspery Ngairo wakati wa mahojiano kuhusu mpango walionao kuwawezesha watu wenye ulemavu na wale wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi

Amesema watu wenye ulemavu wanamchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza shughuli za kimaendelea hapa nchini nakwamba jamii inatakiwa kuondokana na dhana ya kuwa walemavu hawana mchango katika kukuza na kuleta maendeleo ya Taifa.

Aidha Ngairo ameiomba jamii kuondokana na dhana ya kuwa ukimwi una ambukizwa kwa kula ama kuzungumza na mtu mwenye maambukizi hayo na badala yake amewataka kutambua kuwa mtu unaweza kupata maambukizi ya Virusi vya ukimwi kwa kuchangia nyembe, Ngono zembe, kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na Uchangiaji wa damu isiyo salama.

WILAYA YA KILOLO MKOANI IRINGA YAONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO MWAKA HUU.


Halmashauri ya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa imeongeza uzalishaji wa mazao mwaka huu kutokana na wakulima kutumia mbegu bora pamoja na kilimo cha umwagiliaji.

Hayo yamesemwa na Afisa kilimo wa wilaya hiyo Bwana Logan Moses katika maonesho ya kilimo Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Amesema kuwa zao la mahindi limepanda kutoka tani elfu 82 hadi kufikia tani elfu 91 na vitunguu kutoka tani elfu 80 hadi kufikia tani laki moja huku nyanya imepanda kutoka tani laki moja na thelathini na moja hadi kufikia tani laki moja na sitini na tano.

Aidha amewataka wananchi hususani vijana kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuongeza nguvu katika kilimo ili kuleta maendeleo kwa jamii na taifa kwa ujumla.

 BEI YA MAHINDI YASHUKA KWA ASILIMIA 3 WILAYANI MOMBA MKOANI MBEYA.
Bei ya gunia la mahindi imeshuka kutoka shilingi elfu 31 hadi kufikia elfu 28 wakati debe la maharage kushuka kutoka elfu 22 hadi shilingi elfu 18 katika wilaya ya Momba mkoani Mbeya.

Wafanyabiashara na wakulima wa wilayani hiyo wamesema kushuka kwa bei ya mazao kunatokana na kuwepo kwa mavuno mengi .

Mmoja wa wakulima hao Bwana Elius Kaminyoge amesema pamoja na kushuka kwa mahindi na maharage katika soko la majengo pia zao la ulezi limeshuka kutoka shilingio elfu 43 hadi kufikia shilingi elfu 41 kwa gunia na vitunguu kushuka toka shilingi elfu 25 hadi kufikia elfu 18 kwa debe.

Amesema sababu ya kushuka kwa bei ya mazao hayo kunatokana na wakulima kuingiza mazao kwa wingi sokoni hapo.

Kwa hisani ya  CHIMBUKO LETU

Thursday, August 4, 2011

MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI INAZIADA YA TANI MIL 5 YA ZAO LA CHAKULA

Mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini inaziada ya tani milioni 5 za mazao ya Chakula ambazo zitasaidia kulisha mikoa mingine yenye upungufu wa Chakula.

Hayo yameelezwa na naibu waziri wa kilimo, chakula na Ushirikika Injinia Christopher Chiza wakati akifungua maonesho ya kilimo nane nane kanda ya nyanda za juu kusini ambayo yanaendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale vilivyopo kata ya Isyesye jijini Mbeya.

Amesema ziada hiyo ya chakula ni matokeo mazuri yaliyopatikana kutoka kwa wakulima baada ya Serikali kushinikiza wakulima kulima kilimo bora kwa kuzingatia kanuni za kilimo.

Aidha amewataka wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza mkoani Mbeya kwa kufungua viwanda vya usindikaji wa mazao, ambapo kupitia viwanda hivyo wakulima watanufaika kwa kiasi kikubwa katika soko la mazao yao.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile ameiomba Serikali kuwatafutia wakulima soko la ndani na nje ili waweze kunufaika kupitia kilimo.

WAMILIKI WA VITUO VYA MAFUTA JIJINI MBEYA WAGOMEA KUSHUSHA BEI


Wamiliki wa vituo vya mafuta jijini Mbeya wamegoma kushusha bei ya mafuta iliyapangwa na kutangazwa jana na mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji (EWURA.

Uchunguzi uliofanywa katika vituo kadhaa vya mafuta jijini Mbeya umebaini kuwepo kwa mgomo baridi ambapo baadhi ya vituo vimekuwa vikifungwa kwa kisingizio cha kutokuwa na mafuta.

Aidha uchunguzi huo umebaini kuwa katika maeneo mengine vituo vimekuwa vikiendelea kutoa huduma kwa bei ya zamani.

Hapo jana Serikali ilitangaza kushasha bei ya mafuta ili kuwapunguzia makali watumiaji wa badhaa hiyo nchini.

Akizungumza na wanahabari Mkurugenzi wa EWURA bwana HARUNA MASEBU amesema mafuta ya petrol yamepungua kwa shilingi 202 pointi 37 sawa na asilimia 9 nukta 17 ambapo mafuta ya dizeli yatakuwa yamepugua kwa shilingi 173 ambayo ni sawa na asilimia 8

Bwana Masebu alisema alisema bei ya mafuta ya taa imeshuka kwa shilingi 181 nukta 37 sawa na asilimia 8 nukta 70 na mabadiliko hayo yametokana na marekebisho ya yaliyofanywa na kanuni kukokotolea bei za mafuta.

hata hivyo baadhi ya wamiliki wa mafuta mkoani Mbeya wamekuwa wakiuza Petrol 2110 shilingi Dizeli 2015 shilingi na Mafuta ya taa Shilingi 2010.


HUKU NA KULE :- WANAWAKE WAJITOKEZA KUPIMA VIRUSI VYA UKIMWI
Idadi kubwa ya wanawake wamejitokeza kupima virusi vya ukimwi ndani ya viwanja vya John Mwakangale kwenye maonyesho ya nanenane jijini Mbeya yalioanza tarehe mosi Agosti mwaka huu.

Hayo yamesemwa na mmoja wa washauri wa kituo cha kupima na kutoa ushauri nasaha Kihumbe Bi.Eva Lutangilo kuwa wananchi wameonyesha mwamko mzuri kutaka kujua afya zao wakiongoza wanawake.

Ameongeza kwamba licha ya upimaji wanatoa elimu juu ya virusi ukimwi jinsi unavyoambukizwa, dalili zake na jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na ngono.

WANAFUNZI WAJISHUGHULISHA NANE NANE NYAKATI ZA MASOMO.

Baadhi ya Wanafunzi wa shule za msingi jijini Mbeya wameonekana wakijishughulisha na kazi mbalimbali katika uwanja wa maonesho ya kilimo Nane nane badala ya kuwa masomoni.

Watoto hao wamekuwa wakijishughulisha na shughuli za usafi wa mabanda, michezo ya kamali na kubeba mizigo ya baadhi ya wafanyabishara ndogondogo uwanjani humo.

Watoto hao wamekuwa wakionekana kwenye viwanja hivyo muda ambao ni wa masomo huku wakiwa wamevalia sare za shule.

Mtoto Shoham James mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Gombe iliyopo kata ya Uyole amesema ugumu wa maisha na kipato duni cha familia ndio sababu inayowafanya kushindwa kuwa masomoni muda wa masomo na badala yake wanajishughulisha na kazi mbalimbali kwenye maonesho hayo ili waweze kujipatia kipato.

Kwa Hisani ya Mtandao wa BONYEZA HAPA CHIMBUKO LETU

Tuesday, August 2, 2011

MIAKA 50 YA UHURU MKOA WA MBEYA TUMESONGA MBELE

 TUMETOKA MBALI KITUO CHA MABASI MBEYA MIAKA YA 1970,Ktiuo cha mabasi yaendayo mikoani uhindini mbeya enzi hizo za miaka ya 70

                                                 MBEYA IRINGA MIAKA YA 1960
 Hapa ni usangu barabara ya mbeya iringa miaka ya 60,Barabara ilikuwa haina Rami matope kwa sana na ulikuwa na uwezo wa kusafiri Mbeya Iringa kwa zaidi ya siku 2

KWA PICHA HII YA CHINI VIONGOZI WA HALMASHAURI MKOA WAPI KUSIMAMIA SHERIA MLIZOZIWEKA WENYEWE?
Hapa ni uzio wa soko la mwanjelwa linalojengwa wafanya biashara hawalioni tangazo hilo?Hili ni eneo la Mwanjelwa na huo ni uzio uliowekwa wakati ujenzi wa soko la Mwanjelwa ukiendelea.

Sunday, July 31, 2011

MBUNGE WA ILEJE APANIA KUKUZA KIWANGO CHA ELIMU JIOMBINI KWAKE


MBUNGE WA ILEJE ATOA VITAMBU 1000 KUENDELEZA ELIMU JIMBONI KWAKE
Mbunge wa jimbo la Ileje mkoani Mbeya kupitia Chama Cha Mapinduzi ALIKO KIBONA ametoa vitabu elfu moja kwa shule za Sekondari wilayani humo ikiwa ni moja ya ahadi zake katika kuendeleza elimu jimboni kwake.

Akitoa msaada huo mheshimiwa Mbunge KIBONA amesema msaada huo umelenga kupunguza tatizo la vitabu mashuleni ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanafunzi kuwa na uwezo wa kusoma vitabu kwa usía.

Afisa elimu wa wilaya ya Ileje MAY KITIMA ametoa pongezi kwa mbunge huyo kwa kuchangia vitabu elfu moja vitakavyo gawiwa kwa shule 18 za Sekondari ambapo kila shule itapata mgao wa vitabu 50.

Nao madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ileje wameahidi kutoa ushirikiano na mbunge wao kwa kuhimiza wananchi kuchangia shughuli mbalimbali za kimaendeleo hasa katika elimu.

RUVUMA WAJIHIMARISHA KATIKA MAONESHO YA NANE NANE YA KANDA

Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Mkoani Ruvuma imeweka mikakati ya kuwawezesha wakulima kwa kuwapa elimu kuhusiana na kilimo  na ufugaji bora wa wanyama mbalimbali katika maonyesho ya kilimo nyanda za juu kusini kwenye viwanja vya John Mwakangala vilivyopo kata ya Isyesye.

Hayo yamesemwa na bwana GISLA MBUNGU mmoja ya wakulima walio nufaika na mafunzo ya kilimo kutoka wilayani Mbinga katika kijiji cha Mtama.

Bwana Mbungu amesema kuwa mwaka huu wakulima wataelimishwa kuhusiana na uhifadhi wa mazingira katika shughuli zao za kilimo ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo ni changamoto kubwa kwa maendeleo ya kilimo hapa nchini.

Naye ELISI MATESO kutoka kampuni ya DAE LIMITEDI inayojihusisha na uzalishaji wa kahawa wilayani Mbinga amesema kuwa wakulima watapewa mafunzo ya utunzaji miche ya kahawa, usindikaji na matumizi ya zao hilo.

Maonesho ya kilimo nane nane yanaanza kesho katika vinwanja vya JOHN MWAKANGALE

OFISI YA USTAWI WA JAMII YATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUFUATA MISINGI YA SHERIA

SERIKALI imewataka maafisa ustawi wa jamii kubuni miradi mbalimbali itakayoweza kuwasaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kujikwamua katika janga la umaskini.

Hayo yamesemwa jana na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya Moses Chitama wakati akifungua mkutano wa ufunguzi tawi la chama cha Ustawi wa Jamii (Taswa).

Amesema Maafisa wa Ustawi wa Jamii wanatakiwa kuwa chachu ya maendeleo katika jamii inayowazunguka kwa kuwa wabunifu wa miradi ya maendeleo na kufanya kazi kwa moyo moja wa kusaidia watu waishio katika mazingira magumu.

Ameongeza kuwa zimeibuka asasi ambazo zinaangalia maslahi yao wakati wanapewa fedha nyingi na wafadhili kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye matatizo ndani ya jamii.

Amesema ili kuondokana na jamii yenye vijana wanaioshi katika mazingira hatarishi, ofisi ya ustawi wa jamii inatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya utawala na kanuni za kazi zao.

BURIANI MSTAHIKI MEYA WA RUVUMA

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Ali Saidi Manya, Diwani wa kata ya Lizaboni(Mwenye suti Nyeupe) amefariki dunia leo katika Hospitali ya Misheni Peramiho.

Taarifa za Msiba huo zimetangazwa na naibu Meya wa Manispaa ya Songea Mheshimiwa Mariam Dizumba na kupokelewa kwa mshtuko mkubwa na wakazi wa manispaa ya Songea Mkoa wa ruvuma kwa ujumla.

Naibu Meya Dizumba amesema mazishi ya Mstahiki Meya Ali Saidi Manya yatafanywa nyumbani kwake Lizaboni Manispaa ya Songea Siku ya Jumatatu Tarehe 1 Agosti 2011. Maandalizi yanaendelea na wageni kadhaa wa vyeo mbalimbali wamethibitisha kuhudhuria.

WAANDISHI WA HABARI MKOA WA IRINGA WAPATA UTAWALA MPYA

Baadhi ya wanachama wa IPC wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi waliochaguliwa kuongoza IPC ,mwenye pama katikati ni mmiliki wa mtandao huu Bw Francis Godwin ambaye alipita bila kupingwa katika nafasi ya ukatibu msaidizi wa IPC

Katika uchaguzi huu viongozi walioanguka katika uchaguzi huo ambao walikuwemo katika safu ya uongozi katika uongozi uliopita ni pamoja na Sima Bingileki ambaye alikuwa makamu mwenyekiti,huku Eliasa Ally ambaye alikuwa mjumbe kipindi kilichopita akijitoa kugombea tena nafasi hiyo na Kenneth Simbaya akiamua kustaafu nafasi ya kiti pamoja na Hakimu Mwafongo ambaye hakugombea tena nafasi ya ukatibu msaidizi .

Katiba nafasi ya uweka hazina msaidizi Vicky Macha wa Nipashe Iringa alipita bila kupingwa huku nafasi ya katibu msaidizi pia Francis Godwin mwandishi wa gazeti la Tanzania daima Irina ,kurugenzi wa kampuni ya Free Community Media's na mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari za jinsia Tanzania (TGNP) mikoa ya kusini akipita bila kupingwa pamoja na wajumbe 13 7 wa kamati ya utendaji ndani ya IPC pia wakipita bila kupingwa kufuatia Eliasa Ally kujitoa katika kinyang'anyiro hicho.

Wajumbe 13 wanaounda kamati ya utendaji ndani ya IPC ni pamoja na Daud Mwangosi, Frank Leonard ,Zulfa Shomary, Francis Godwin, Suleman Boki,Vicky Macha, Getrude Madembwe, Shabani Lupimo, Frederick Siwale,Conard Mpila,Fulgence Malangalila,Janeth Matondo na Jackson Manga .

KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM CHAFUNGULIWA LEO MJINI DODOMA, AMBAPO MENGI YANATARAJIWA KUJITOKEZA KTK KIKAO HICHO

Mwenyekiti wa CCM taifa, Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar, Aman Abeid Karume (wa tatu kushoto), Rais wa Zanzibar, Dkt Ali Mohamed Shein na Mwenyekiti wa CCM Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi (kushoto), Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa (kulia) na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Willson Mukama, wakiwa katika ufunguzi wa Kikao cha Kamati kuu kilichofunguliwa leo Julai 31, katika Ukumbi wa CCM Makao Makuu mjini Dodoma. 
 Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, akiingia katika Ukumbi wa CCM Makao Makuu mjini Dodoma, leo Julai 31, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Kamati kuu. Kulia ni Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Willson Mukama
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika ufunguzi wa Kikao cha Kamati Kuu kilichoanza leo Julai 31, 2011 katika Ukumbi wa CCM Makao Makuu mjini Dodoma. Katikati ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

WAANDISHI WA HABARI MACHACHARI MKOANI MBEYA KWA MWAKA 2007


Hawa ni waandishi  wa habari mkoani mbeya kwa miaka minne iliyopita wakiwa nje ya Ukumbi wa Mkutano wa MKAPA uliopo jijini Mbeya na kupiga picha ya pamoja.

Ukiwa tazama siku hizi ni tofauti na maumbile yao walivyokuwa hapo awali, Je? Nini maoni yako?

Saturday, July 30, 2011

WAZAZI WAPINGA KITENDO CHA KUTOA MCHANGO WA CHAKULA MBATA JIJINI MBEYA

Wazazi wa mtaa wa Mbata kata ya Ghana jijini Mbeya wamepinga kitendo cha kutoa mchango wa chakula kwa wanafunzi sio kigezo cha kuboresha kiwango cha kufaulu kwa wanafunzi katika shule za msingi.

Wakijadili katika mkutano wa wazazi uliofanyika shule ya msingi Mbata wazazi hao wamesema wizara ya elimu inatakiwa kuangalia njia nyingine inayoweza kuwafanya wanafunzi kumudu masomo yao na si kwa kutumia kigezo cha chakula mashuleni.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Mbata Agabo Mwakatobe amewataka wazazi kuchangia gharama za chakula kwa watoto wao kwa kuwa wanafunzi wanapokuwa na njaa hawatoweza kusikiliza wanachofundishwa na waalimu wao.

Hivi karibuni wananchi waliilalamikia Serikali kushindwa kutoa chakula mashuleni, lakini baada ya Serikali kukubali mpango wa chakula mashuleni wazazi wameanza kupingana kuhusu mpango huo.


HALI YA MIUNDOMBINU BADO NI TETE MBEYA VIJIJINI
Wakazi wa vitongoji vya DDC, Mtakuja na Mlima Reli wilaya ya Mbeya Vijijini wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 7 kutafuta huduma ya maji safi na salama.

Wakazi hao wamesema kutokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama wamekuwa wakilazimika kutumia maji ya Mto Mbalizi ambayo maji yake ni machafu na sio salama kwa matumizi ya binadamu.

Mmoja wa wanakijiji hao Michael Mwaifwani amesema licha ya kuwepo kwa miundombinu ya maji katika vitongoji hivyo bado upatikanaji wa huduma hiyo imekuwa ni tabu na kwamba wamekuwa wakilazimika kulipa bili ya maji ya shilingi elfu kumi kila mwezi.

Naye mwenyekiti wa kitongoji cha DCC bwana Joined Mwalusanya amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa ongezeko la wakazi ni moja ya sababu inayopelekea utoaji wa huduma hiyo kusua sua. 


BEI ZA MAZAO ZA BADIRIKA MARA KWA MARA SOKO LA SIDO MWANJELWA MBEYA.
Bei za mazao ya vyakula katika soko la Sido Mwanjelwa jijini mbeya zimekuwa zikibadilika mara kwa mara kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji.

Mmoja wa wafanyabishara sokoni hapo bwana James Fredrick amesema debe la nyanya imepanda kutoka shilingi elfu 10 hadi kufikia shilingi elfu 12 kwa sasa.

Naye Lugano Mwakalundwa amesema bei ya mahindi imepanda kutoka shilingi elfu 33 kwa gunia hadi kufikia shilingi elfu 36 na kwamba kuna uwezekano wa bei hiyo kuendelea kupanda kutokana na mahitaji makubwa ya chakula hicho kwa mikoa mingine ambayo inakabiliwa na tatizo la njaa.


Kwa hisani ya CHIMBUKO LETU Bloguhttp://ukurasampyahuu.blogspot.com/ 

Friday, July 29, 2011

JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA KUENDELEA KUFANYA UCHUNGUZI WA MGOGORO

JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA KUENDELEA KUFANYA UCHUNGUZI WA MGOGORO
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Mbeya ADVOCATE NYOMBI amesema jeshi lake linaendea na uchunguzi ili kubaini ukweli wa mgogoro kati ya wananchi wa kijiji cha kapunga wilayani Mbarali mkoani Mbeya dhidi ya mwekezaji wa kampuni Rice Project

Kuhusu vitendo vya uharibifu wa mali za wananchi Kamanda NYOMBI amesema hana taarifa nazo na kwamba na kuwataka wananchi hao kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea.

Hata hivyo habari tulizozipata zinadai kuwa mwekezaji huyo alivunja matofali kumi na mbili elfu ambayo yalifyatuliwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi Mbarali na kumjeruhi mwanakijiji kwa kumgonga na gari.
 
MAITI YA MTOTO MCHANGA YATUPWA JALALANI MBEYA.
Maiti ya mtoto mchanga imekutwa ndani ya mfuko wa Rambo uliotupwa kwenye dampo la shule ya msingi ya Sinde liliyopo kata ya Ruanda mtaa mtoni jijini Mbeya.

Habari za kukutwa kwa maiti ya mtoto mchanga zimetolewa na watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi ambao walikuwa wanaokota mifuko hiyo kwenye dampo hilo kwa ajili ya kwenda kuziuza kwa wafanyabiashara wa mkaa.

Imeeleza kuwa baada ya watoto hao kuifungua Rambo ndipo walipokutana na maiti ya mtoto mchanga na kutoa taarifa kwa wafanyabiashara na wakazi wa mtaa wa Mtoni ambao nao walitoa taarifa kwa jeshi la polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Hata hivyo hakuna mtu anayehisiwa kwenye mtaa huo kuhusika na tukio la kutupwa kwa maiti hiyo, Jeshi la polisi lilifika eneo hilo majira ya saa mbili za usiku na kuondoka na mwili wa mtoto huyo ambaye anadaiwa kuwa na siku moja tangu azaliwe.

UKOSEFU WA VITENDEA KAZI KITUO CHA AFYA NSONYANGA - MBARALI
Kituo cha afya cha Nsonyanga kilichopo kijiji cha Kapyo kata ya mahongole wilayani mbarali mkoani Mbeya kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vitendea kazi, usafiri kwa ajili ya wagonjwa, nyumba za watumishi na upatikanaji wa nishati ya umeme.

Mkuu wa kituo hicho Dakta EDSON MWANDEUKA amesema wanalazimika kutumia taa ya Chemli wakati wa kutoa huduma za uzazi kwa wakina mama wajawazito nyakati za usiku hali inayohatarisha usalama wa afya kwa wakina mama hao.
Kutokana na tatizo hilo mwenyekiti wa kijiji hicho bwana KYANDO amesema uongozi wa kijiji chake unaendelea na mchakato wa kufanikisha kituo hicho kinapata nishati ya Umeme ili kurahisisha zoezi la utoaji wa huduma kwa wagonjwa nyakati za usiku.

Kituo cha Nsonyanga kina wauguzi 3 ambapo kituo hicho kinahudumia vijiji vya kapyo, uswisi, ilongo, Nsonyanga, azimio mapula, malawato na mkoi.

MAONYESHO YA KILIMO MWAKA HUU MKOANI MBEYA YAVUNJA REKODI.
Maonesho ya Kilimo ya mwaka huu yamevunja rekodi ya mwaka jana baada ya kujitokeza wadau wapatao 400 watakaoshiriki kwenye maonesho hayo ikilinganishwa na ya mwaka jana ambayo wadau takriban 300 ndio walioshiriki maonesho hayo.

Kwa upande wa miundo mbinu KASILATI amesema TASO imejiandaa kuhakikisha barabara zinachongwa vizuri, huduma za Afya zinatolewa uwanjani humo, maji yanapatikana licha ya changamoto ya nishati ya Umeme kuwepo.

Aidha Bwana KASILATI ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo yatakayoanza rasmi tarehe moja mwezi wa Nane.

UZOAJI TAKATAKA WAENDELEWA KUSUASUA MJI MDOGO WA MBALIZI MBEYA VIJIJINI.
Wafanyabiashara wa soko la Tarafani Mbalizi Wilaya ya Mbeya vijijini wameulalamikia uongozi wa soko hilo kwa kushindwa kutoa takataka zilizojaa kwenye Dampo la soko hilo kwa mda mrefu.

Wamesema halmashauri ya wilaya hiyo haina utaratibu wa kuzoa na kutupata taka pindi zinapo jaa kwenye dampo hali inayopelekea kuwepo kwa harufu mbaya sokoni hapo.

Mmoja wa wafanyabishara wa soko hilo RASHIND EFRAIMU amesema wamekuwa wakilipia ushuru kila siku na kwamba kinachowakera ni kuona takataka zikiendelea kurundikana kwenye dampo ikiwa ni pamoja na miundombinu ya soko kuendelea kuwa mibovu.

Nao wauzaji wa chakula wameuomba uongozi wa halmashauri ya Mbeya Vijijini kuchukuwa hatua za haraka za kuondoa taka kwenye madampo ili kuondoa kero ya harufu mbaya inayopelekea kukimbiwa na wateja.

Afisa afya wa soko hilo MHEMEJI amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa uchache wa magari ya kubebea taka ndio sababu ya kusuasua kwa zoezi la uzoaji wa taka.

Kwa hisani ya CHIMBUKO LETU Blogu http://ukurasampyahuu.blogspot.com/

Thursday, July 28, 2011

VITUKO BUNGENI JAMANI SI VYA KUVIFUMBIA MACHO KAMA WANANCHI

 Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA) Ezekia Wenje (aliyevaa suti ya rangi ya maziwa) akitolewa nje ya ukumbi wa Bunge na Askari Polisi wa Bunge baada ya kutomtii Mwenyekiti wa kikao cha Bunge cha leo Mbunge wa Dole (CCM) Silvester Mabumba, alimtaka kukaa chini na kutokutoa hoja ya dharula kuhusu Samaki wa sumu kutoka
 Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA) Ezekia Wenje (aliyevaa suti ya rangi ya maziwa) akitolewa nje ya ukumbi wa Bunge na Askari Polisi wa Bunge.
 Mbunge wa Ludewa (CCM) Deo Filikunjombe (kushoto) akisutwa nje ya ukumbi wa Bunge na baadhi ya wabunge wa upinzani Moses Machari (kulia), Philipa Mturano (katikati) na Ezekia Wenje (kushoto) baada ya Filikunjombe kumwambia Wenje kuwa alikosa ustaarabu kwa kutokumtii Mwenyekiti wa kikao cha Bunge cha leo Mbunge wa Dole (CCM) Silvester Mabumba pale alipomwambia akae chini na kutokutoa hoja ya dharula kuhusu samaki wa sumu kutoka Japan.
 Baadhi ya mawaziri wakimpongea waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Prof. Jummanne Maghembe mara baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya wizara yake jana jioni katika kikao cha Bunge la bajeti kinachoendelea mjini Dodoma.

                                                              NJE YA UKUMBI WA BUNGE
 bunge wa Ludewa (CCM) Deo Filikunjombe (kushoto) akisutwa nje ya ukumbi wa Bunge na Mbunge wa viti Maalum (CHADEMA) Suzan Kiwanga (aliyevaa kitenge) baada ya Filikunjombe kumwambia, Ezekia Wenje, mbunge wa Nyamagana (CHADEMA) (hayupo pichani) alikosa ustaarabu kwa kutokumtii Mwenyekiti wa kikao cha Bunge cha leo Mbunge wa Dole (CCM) Silvester Mabumba pale alipomwambia akae chini na kutokutoa hoja ya dharula kuhusu Samaki wa sumu kutoka Japan.
Mbunge wa Ludewa (CCM) Deo Filikunjombe (kulia) akisutwa nje ya ukumbi wa Bunge na wabunge wa viti Maalum (CHADEMA) Philipa Mturano (kushoto) Suzan Kiwanga (aliyevaa kitenge) na Mbunge wa jimbo la Kasulu mjini (NCCR – MAGEUZI) Moses Machari.

WANAFUNZI WAGEUZWA NAWAALIMU KUWA WAFANYAKAZI WA NDANI MAENEO YA VIJIJINI

 Wanafunzi wa shule ya Msingi Manda wilaya ya Ludewa wakitoka kuokota kuni za kuuza ili kupata fedha za mchango wa mitihani
 Wanafunzi wa kike katika shule ya msingi Manda wilaya ya Ludewa ambao wanasubiri kufanya mtihani wa Taifa wa Darasa la saba wakitoka kuokota kuni porini mida ya masomo baada ya kufukuzwa kwa kushindwa kulipa mchango wa shilingi 600 ili wapate kufanya mitihani ya kujipima ya kata mzigo wa kuni kama huu wamekuwa wakiuuza kwa kiasi cha shilingi 100 kwa walimu wao
Afisa elimu wa wilaya ya Ludewa Bw.Yella akiwahoji wanafunzi shule ya msingi Manda ambao walikutwa wakitoka kuvua samaki wakati wa masomo baada ya kufukuzwa na walimu kwa kushindwa kulipa mchango wa shilingi 600 wa mtihani wa kata
Wakati haya yakijitokeza huko Ludewa jamii inatakiwa kijitathimini mara mbili kuangalia namna ambavyo tunaweza kudhibiti vitendo hivyo ili kuwawezesha wanafunzi kutumia muda wao vizuri ktk masomo yao

UONGOZI WA CHIMALA SACCOS HAUTENDI HAKI WAKATI WA KUTOA MIKOPO,

Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wamesema uongozi wa Chimala Saccos umekuwa hautendi haki wakati wa kutoa mikopo kwa wananchi na badala yake wamekuwa wakiutumia ushirika huo kujinufaisha wao na familia zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao cha Baraza la Madiwani wamesema kuwa sehemu kubwa ya mkopo wa shilingi bilioni 4 umewanufaisha viongozi wa Ushirika huo na sio wananchi.

Wakitoa azimio la pamoja chini ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo KENETH NDINGO Wametaka kufanyika kwa ukaguzi wa vitabu vya Saccos wilayani humo ili kudhibiti vitendo vya baadhi ya viongozi wa Ushirika kujinufaisha wao na familia zao.

Awali Ofisa Ushirika wa wilaya ya Mbarali John Manyama, amesema Chimala saccos inazo hisa zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni sitini na tano na laki saba akiba ya zaidi ya shilingi milioni mia nne sitini na tisa elfu na amana ya zaidi ya shilingi milioni sitini na mbili.

Kwa mujibu wa Manyama mikopo iliyotolewa na Chimala saccos hadi sasa ni zaidi ya shilingi milioni 4 na kwamba marejesho hadi sasa ni zaidi ya shilingi milioni 3 huku kiasi cha mkopo ambacho bado hakijarejeshwa ni zaidi ya bilioni moja.

MANDAMANO YA WANANCHI KATA YA UTENGULE USANGU - MBARALI.
Zaidi ya wakazi 80 wa kata ya Utengule Usangu iliyopo wilayani Mbarali wameandamana hadi ofisi ya Diwani wa kata hiyo kupinga kuhamishwa kwa Dakta Joseph Megafu kutokana na mchango wake katika kituo cha Afya cha Utengule.

Wamesema dakta huyo anamchango mkubwa katika kutoa huduma kwa akina mama na watoto na kwamba kuhamishwa kwake kunaweza kuzorotesha utoaji wa huduma kwa kundi hilo muhimu ndani ya jamii.

Aidha inadaiwa kuwa mpango wa kuhamishwa kwa dakta huyo unatokana na umakini alionao katika kusimamia huduma kwa jamii.

Naye Diwani wa kata hiyo Juntiva Mwalyaje amepokea malalamiko hayo na kuwataka kuwa watulivu wakati akiliwasilisha ombi lao kwa mganga mkuu wa wilaya ambaye ndiye mwenye dhamana ya kumrejesha Dakta JOSEPH MEGAFU kuendelea kutoa huduma katika kituo hicho cha afya.

USAFI WA MAZINGIRA KATA YA ILEMI JIJINI MBEYA.
Juhudi za vyombo vya habari kwa kushirikiana na uongozi wa kata ya Ilemi jijini Mbeya kutoa elimu ya usafi wa mazingira, wakazi wa Mtaa wa Mwafute wameanza kuchukua hatua ya kusafisha maeneo yao ikiwa ni pamoja na kujenga Ghuba za kuhifadhia taka.

Afisa mtendaji wa kata hiyo Bwana Stivu Mwamboneke amesema baada ya vyombo vya habari kuhamasisha usafi wa mazingira wakazi wa eneo hilo wamekuwa na mwamko wa kusafisha mazingira yanayo wazunguka ikiwa ni pamoja na kuzuia maji machafu kutiririka kwenye mto  Jihanga.

Aidha amewaomba waandishi wa habari kutembelea maeneo hayo ili kuwahamasisha wakazi hao kuendeleza usafi wa mazingira na kukarabati vyoo vyao. 

WIZI NA ULINZI KATA YA SINDE JIJINI MBEYA.
Wakazi wa mtaa wa Janibichi kata ya Sinde jijini Mbeya wanaishi kwa wasiwasi mkubwa wa kuvunjiwa nyumba zao kisha kuibiwa vitu vya thamani kutokana kuibuka kwa vitendo vya wizi mtaani hapo.

Mwenyekiti wa mtaa huo Bwana Joel Kitwika amesema wizi huo hufanywa nyakati za usiku wakati wengine wakiwa wamelala ndipo wezi hao hupata nafasi ya kuiba baadhi ya vitu na mifugo kama kuku na bata.

Aidha amewataka wakazi wa mtaa huo kuweka ulinzi wa jadi (Sungusungu) ili kudhibiti vitendo hivyo na kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi pindi wanapohitajika kuunda kikosi cha Sungusungu kwenye mtaa wao.

Kwa hisani ya mtandao wa (Link Here) http://ukurasampyahuu.blogspot.com/ UKURASA MPYA HUU

Wednesday, July 27, 2011

WAAFRIKA WAHUSISHWA NA MAUAJI YA PAKISTAN

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan amesema baadhi ya raia wa Kiafrika wamehusika katika machafuko ya hivi karibuni huko katika mji wa Karachi makao makuu ya mkoa wa Sindh. 

Rahman Malik amesema baadhi ya raia wa Kiafrika wanashukiwa kuhusika katika machafuko na mapigano ya hivi karibuni katika mji wa Karachi na kueleza kuwa vikosi vya usalama vya Pakistan vimetayarisha orodha ya majina ya raia hao wa Kiafrika waliohusika kwenye machafuko. Amesema hivi sasa hawawezi kutaja majina ya nchi za Kiafrika wanapotoka watu hao na kuongeza kuwa kwa kushirikiana na idara za usalama wa taifa za nchi hiyo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Pakistan ina mpango wa kuwafungulia mashtaka wale wote wanaoshukiwa kuhusika katika machafuko hayo ya Karachi. Watu wasiopungua 25 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mapigano yaliyojiri hivi karibuni katika mji wa Karachi huko Pakistan kati ya muungano wa umoja wa kikabila na harakati ya wageni wahamiaji nchini humo.

Tuesday, July 26, 2011

BENKI YA CRDB MBEYA YATOA MKOPO WA MILIONI 300 KWA WAKULIMA

 Benki ya CRDB tawi la mbeya imetoa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 300 kwa wakulima wadogowadogo wa chai wa wilaya ya Rungwe ili waongeze uzalishaji wa zao hilo.

Hayo yamebainika wakati wa uzinduzi wa ofisi ya chama cha akiba na mikopo SACOSS cha wakulima hao.Kaimu meneja wa benki hiyo JOHNSON MWANSOJO amesema kuwa mkopo huo utaiwezesha SACOSS hiyo kutoa huduma za kibenki. Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika kata ya Kandete mwakaleli MWANSOJO amesema mkopo huo utanufaisha wakulima wazao wapatao elfu 15. MWANSOJO amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa tawi hilo ni kuwajengea uwezo wakulima kupata fedha zao za malipo ya mazao ya kilimo na kuwaepusha kutembea umbali mrefu kutafuta malipo hayo. Amesema hiyo ni mikakati ya CRDB kuhakikisha inawajengea uwezo wakulima na kujikita zaidi katika uzalishaji wa chai na kuwawezesha kupata mikopo kwa uraisi kupitia SACOSS yao ili kujikwamua na umaskini

HABARI HII NI KWA HISANI YA http://ukurasampyahuu.blogspot.com/

Sunday, July 24, 2011

Afisa ushirika jiji la Mbeya BUMI MASUBA ameusimamisha kazi uongozi wa Ilomba market Saccos kwa kipindi cha wiki 2

Afisa ushirika jiji la Mbeya BUMI MASUBA ameusimamisha kazi uongozi wa Ilomba market Saccos kwa kipindi cha wiki 2 ili kupisha uchunguzi dhidi yao wa shilingi Milioni 22 fedha ambazo zimetumika katika mazingira ya kutatanisha.

Akihitimisha mjadala uliodumu kwa zaidi ya masaa mawili Afisa ushirika aliwataka wanachama wa Ilomba Market Saccos kuchagua wajumbe watano watakao simamia uchunguzi, ambapo kamati ya Muda itakuwa na jukumu la kuwasilisha mahesabu ofisi ya halmashauri ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kwa wahusika endapo kutabainika kuwepo kwa ubadhilifu wowote wa fedha za umoja.

Walichaguliwa na wajumbe walio udhuria mkutano huo ni ALLY UHA, EVARISTO PANGANI, NDUMIGWE KAJIGIRI, BEATRICE RUASI na AGUSTINO KAPANGA.

Inadaiwa kuwa uongozi uliosimamishwa kazi chini ya Uwenyekiti wa SANGA J.SANGA ulikopa shilingi milioni 136 toka NMB na ukakopesha milioni 72 kwa wanachama wake ambapo shilingi milioni 19 zinadaiwa zimerejeshwa na shilingi milioni 31 zikiwa hazijarejeshwa hata hivyo taarifa haioneshi matumizi ya shilingi miolioni 22.

Ilomba Market Saccos inajumla ya wanachama 200 ambapo kati yao wanachama hai ni 150

Nzovwe - Jijini Mbeya.

Chuo cha maendeleo ya wananchi kilichopo kata ya Nzovwe wilaya ya Mbeya kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi hasa waalimu wa fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na masomo ya uelewa.

Akiongea katika tafrija fupi ya kuwaaga wanafunzi iliyofanyika chuoni hapo jana mkuu wa chuo hicho Bi REHEMA ASUKULYE amesema walimu waliopo ni watatu hali inayowalazimu kutafuta waalimu kutoka vyuo vingine.

Ameongeza kuwa pamoja na upungufu wa waalimu pia chuo kinadaiwa na idara ya maji shilingi milioni mbili na nusu kwa ajili ya kulipia ankra ya maji.

Kutokana na changamoto hizo ameiomba Serikali kukisaidia chuo hicho ili kiweze kukabiliana na madeni yanayowakabili.

DANNY MWAKITELEKO WA NEW HABARI COORPORATION AAGA DUNIA AACHA SIMANZI KWA WANAHABARI NCHINI TANZANIA

 NAIBU MHARIRI MTENDAJI wa Kampuni la New Habari Coorporation (2006) Limited, Danny Mwakiteleko amefariki dunia mapema leo majira ya saa 10 Alfajiri katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
 Dany Akiendelea kupata matibabu mara baada ya Kupata ajali ya Gari iliyompelekea kufanyiwa Oparesheni ya Kichwa hata Hivyo mwenyezi Mungu alimpenda zaidi na hivyo kumtwaa jana alfajiri na anatarajiwa kuzikwa Wilayani Rungwe mkoani Mbeya siku ya Juma Nne
Gari lilianzisha Safari ya Maisha mapya ya Dany Kitwana.
DANNY MWAKITELEKO HATUNAE TENA DUNIA BALI NI HISTORIA TU


ALIYEKUWA Mhariri  wa gazeti la Rai, ambaye pia ni Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari, Danny Mwakiteleko , amefariki dunia leo alfajiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na anatarajiwa kuzikwa kesho kutwa wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Mwakiteleko alilazwa katika kitengo cha watu mahtuti Muhimbili baada ya ajali aliyoipata usiku wa jumatano wiki hili eneo la Tabata na kukimbizwa katika Hospitali ya Amana, Ilala na baadaye Muhimbili.

 Katika ajali hiyo gari alilokuwa akiendesha Mwakiteleko liligongwa na lori lenye trela, ambalo lilitoweka bila kujulikana saa nne usiku. Mwakiteleko alikuwa akitokea kazini Sinza ambako alifanya kazi hadi saa tatu usiku.

Jana Rais Jakaya Kikwete alienda kumuona na kuelezwa kwamba hali yake inaendelea vyema.

Danny Mwakiteleko, amefariki dunia akiwa  na umri wa miaka 45 na anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Rugombo, Mwakaleli wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Saturday, July 23, 2011

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA MHESHIMIWA BERNAD MEMBE (MB)AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012

                                   WAZIRI MHE. BERNARD KAMILLIUS MEMBE
A. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

2. Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nachukua fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne. Pili, ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kunichagua kwa mara nyingine tena kuongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Aidha, ninampongeza Dkt. Mohammed Gharib Bilal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, ninampongeza Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, (Mb.) kwa kuchaguliwa bila kupingwa kuwa Mbunge na kuteuliwa tena na Mhe. Rais na hatimaye kuthibitishwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Waziri Mkuu kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne.

3. Mheshimiwa Spika, napenda nikupongeze kwa kuchaguliwa kwa kishindo kushika nafasi ya Spika wa Bunge letu tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu, miaka 50 iliyopita. Uteuzi wako ni kielelezo cha ukomavu wa demokrasia ya nchi yetu na imani kubwa tuliyonayo sisi Waheshimiwa Wabunge, juu ya utendaji wako uliotukuka. Kadhalika, nampongeza Naibu Spika, Mhe. Job Ndugai pamoja na Wenyeviti kwa kuchaguliwa katika kusaidia uendeshaji wa Bunge hili tukufu. Napenda pia kuwapongeza Mawaziri wenzangu pamoja na Naibu Mawaziri wote, kwa kuteuliwa kwao na Mhe. Rais kushika nyadhifa hizo. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupata heshima na dhamana kubwa ya kuwawakilisha wananchi wa majimbo pamoja na makundi mbalimbali ya jamii katika Bunge hili.
4. Mheshimiwa Spika, naomba kwa namna ya pekee niwashukuru Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) na Waziri wa Fedha, Mhe. Mustafa Haidi Mkulo (Mb.) kwa hotuba zao ambazo zimetoa mwelekeo wa Taifa letu katika mwaka huu wa fedha. Hotuba zao zimegusia mambo ya kimsingi yanayohusu Wizara yangu. Naomba pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Mawaziri wenzangu wote walionitangulia katika kuwasilisha hotuba zao kwa kuzungumzia kwa ufasaha baadhi ya masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa wanayoyashughulikia katika Wizara zao. Wizara yangu imekuwa ikishirikiana vyema na kwa karibu sana na Wizara hizi, na mara zote imekuwa ikizingatia ushauri wao kwa umakini mkubwa.

5. Mheshimiwa Spika, napenda pia niwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya Uenyekiti wa Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.) kwa ushauri wao ambao umekuwa wa msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu ya Wizara yangu kwa mafanikio.

6. Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye ameendelea kuwa wa msaada mkubwa kwangu katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Aidha, namshukuru Katibu Mkuu, Bwana John M. Haule; Naibu Katibu Mkuu, Balozi Rajabu Gamaha, Wakurugenzi wote, Mabalozi wetu pamoja na wafanyakazi wenzangu wote Wizarani na katika Balozi zetu kwa bidii na kujituma kwao ipasavyo katika kutetea na kulinda maslahi ya nchi yetu ndani na nje na pia kwa kufanikisha kwa wakati hotuba hii ya bajeti.

7. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wapiga kura wangu na wananchi wa Jimbo la Mtama, kwa upendo wao na imani yao kwangu. Napenda pia niwashukuru viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wa Mkoa wa Lindi kwa uongozi thabiti na kwa ushirikiano wao mkubwa. Kwa upande wa familia yangu, ningependa kumshukuru sana mke wangu, Dorcas Membe, pamoja na watoto wetu kwa kunitia moyo na nguvu katika shughuli zangu za kila siku. Mama Membe hayupo pale juu leo kwa sababu yupo nje ya nchi akimuuguza kijana wetu Denis ambaye amefanyiwa upasuaji mkubwa na namtakia afya njema.




B. HALI YA DUNIA NA CHANGAMOTO ZILIZOPO

8. Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi na usalama duniani kwa ujumla ni shwari isipokuwa katika maeneo machache ambayo yanahitaji uangalizi wa makini wa jumuiya ya kimataifa.

9. Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi katika nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, imeendelea kuimarika baada ya kipindi kigumu cha mdororo wa uchumi uliyoikumba dunia mwaka 2008 licha ya baadhi ya nchi kama Ugiriki, Uhispania na Ureno kuendelea kusuasua katika kuimarisha uchumi wao. Kwa ujumla, hali ya usalama duniani inatia moyo ingawa kuna maeneo machache ambayo yamegubikwa na migogoro ya ndani, iliyosababishwa na shinikizo la kutaka mabadiliko ya kisiasa, kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa ajira. Hali hiyo imeleta madhara makubwa katika nchi ambazo hazikuingia katika mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaliyoanza katika miaka ya themanini hadi miaka ya tisini. Madhara hayo ni pamoja na vifo vya raia, ongezeko la wakimbizi, uharibifu wa miundombinu, kuzorota kwa shughuli za uzalishaji na hivyo kuongezeka kwa umaskini na hatari ya kuibuka kwa vitendo vipya vya kigaidi. Wizara yangu imeendelea kufuatilia na kushiriki kikamilifu katika michakato ya kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro hiyo.

MATUKIO YA MAUAJI NA UNYANYASAJI DHIDI YA WANAWAKE SASA NI KERO MBEYA

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ADVOCATE NYOMBI akitoa taarifa ya matukio ya Ujambazi na mauaji mkoani Mbeya hapo alikuwa Mbele ya waandishi wa Habari
VITENDO HIVI VYA UNYANYASAJI WANAWAKE VISIPO CHUKULIWA HATUA ZA HARAKA TUNAHATARI YA KUSABABSHA VIFO VINGI KWA WANAWAKE NA WATOTO
MBEYA
WATU watatu wamefariki dunia mkoani Mbeya katika matukio tofauti mmoja kwa kukatwa na shoka kichwani, mwingine kwa kukatwa koromeo na kutobolewa macho huku wa tatu akiwa ameuawa kutokana na wivu wa mapenzi.

Tukio la kwanza limetokea eneo la kijiji cha Isalilo wilayani Mbozi ambapo Amina Maonezi Tuliaje (18) ambaye alikuwa Mkulima aliuawa kwa kukatwa na shoka kichwani na Nemes Muyombe ambaye ni mumewe na marehemu.

Baada ya tukio hilo shoka lililotumika katika mauaji hayo liling'ang'aniwa kichwani ambapo sababu ya mauaji hayo imeelezwa kuwa ni kupakuliwa mboga kidogo na baada ya mauaji hayo mtuhumiwa alitoroka kusikojulikana.

Tukio la pili lilitokea katika kijiji cha Isaka kata ya Nkunga wilaya ya Rungwe ambapo Alex Hezron (22) aliyekuwa mkazi wa eneo la Igogwe aliuawa kwa kukatwa koromeo lake na watu wasiofahamika ambapo mwili wake ulikutwa na majeraha mengine matatu kichwani na kisogoni.

Mwili wa marehemu huyo ulikutwa umetobolewa macho yote mawili na mwili wake ulikutwa eneo la mto Igogwe na kwamba Maerehemu alitoweka nyumbani tangu Julai 18 mwaka huu.

Katika tukio la tatu lililotokea eneo la Uturo wilaya ya Mbarali Ombeni Msigwa (31) kabila Mbena alifariki dunia akiwa anakimbizwa Hospitalini baada ya kupigwa na mumewe aitwaye Siasa Njali (32) ambapo chanzo cha mauaji hayo kimeelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi ambapo alikuwa akituhumiwa kuwa na mahusiano na wanaume wengine.

Matukio yote hayo yamethibitishwa na Kamanda wa polisiwa mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi ambaye amesema kuwa katika matukio hayo mtuhumiwa mmoja wa tukio la mauaji ya wivu wa kimapenzi amekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa na jeshi hilo.

MAANDALIZI YA SIKU YA MASHUJAA MBEYA YAENDELEA VIZURI MBEYA

 Jiwe la msingi lenye majina ya mashujaa waliokufa vitani eneo la uhindini kama linavyoonekana katika makaburi yaliyopo eneo hilo.
 Askari wa JWTZ kikosi cha 44 KJ wakiwa kwenye mazoezi ya maandalizi ya siku ya mashujaa mkoani Mbeya leo.

DK.SLAA APINGWA NA MADIWANI WAKE KUHUSU AGIZO LA KUJIHUZURU NYADHIFA ZAO

 CHADEMA YAPANGARUKA, KILA MMOJA ATAKA KUONEKANA MBABE DHIDI YA MWENZAKE:
MADIWANI watatu wa Chadema waliotakiwa kujiuzulu nyadhifa zao katika Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kufikia saa 7:02 mchana jana, wamegoma kufanya hivyo na badala yake wameutaka uongozi wa taifa wa chama hicho kuwasafisha kwa kuwataka radhi.

Kauli hiyo ya madiwani hao akiwamo Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Estomi Mallah imekuja siku chache baada ya kuvuja kwa ripoti ya kamati iliyoundwa na Chadema kuchunguza mwafaka wa madiwani wake, wa CCM na TLP katika kumpata Meya wa jiji hilo ikibainisha kuwa hakukuwa na tuhuma za rushwa katika mchakato huo.

Badala ya kujiuzulu, madiwani hao wametoa masharti magumu kwa chama hicho, licha ya kutaka kusafishwa, pia wamemtaka Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuwasafisha kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kueleza umma kwamba hawakuhongwa.

Mallah ambaye ni mwenyekiti wa madiwani hao alisema jana kuwa wamekitaka chama chao kuwaomba radhi kupitia vyombo vya habari kwa kuwa ripoti hiyo imebainisha ukweli wa mambo. Alisema taarifa za wao kuhongwa zilizotolewa na uongozi wa chama chao ziliwasababishia usumbufu mkubwa ndani ya jamii zao kiasi cha kufanya baadhi yao kunusurika kupigwa mawe.

Akizungumzia agizo la kujiuzulu nyadhifa ndani ya manispaa hadi kufikia jana saa 7:02, alisema wamepanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa kuwa hawakutendewa haki. Mallah aliutaka uongozi wa Chadema kutambua misingi ya haki huku akibanisha kuwa migogoro ya ndani kwa ndani huenda ikakipeleka mahali kubaya akisema kama kuna tatizo, linapaswa kutatuliwa kupitia vikao na si vinginevyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Elerai (Chadema), John Bayo alikwenda mbali akimtaka Lema kupita katika maeneo yote ya Jiji la Arusha kuwasafisha mbele ya wananchi kutokana na tuhuma alizozitoa kuwa walipokea rushwa.

Chadema kimetofautiana na madiwani hao kwa kile inachoeleza kuwa wamepingana na msimamo wa chama hicho kutotambua mwafaka katika mgogoro wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapinga jinsi muafaka huo ulivyofikiwa kikisema haukufuata misingi ya kisheria ba kwamba ili mwafaka upatikane mambo kadhaa yalipaswa kujadiliwa kwa pamoja ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa chama hicho kutokana na maandamano yaliyofanyika mapema mwaka huu kupinga matokeo ya uchaguzi wa meya, kulipwa fidia kwa familia za marehemu waliokufa kwenye maandamano hayo na uchaguzi wa meya wa jiji hilo kurudiwa.

Uongozi wa taifa wa chama hicho unaona kwamba kitendo cha madiwani hao kukubali nyadhifa ndani ya Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha kabla mambo hayo hayajatekelezwa, kimetafsiriwa na Kamati Kuu ya Chama hicho kuwa ni usaliti uliotokana na rushwa.

Wahudhuria kikao cha halmashauri ya jiji

Licha ya madiwani hao kupuuza agizo hilo la makao makuu ya Chadema, jana walihudhuria kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kikifanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kama kawaida huku baadhi yao wakisema sasa wameamua kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi waliowachagua ili kuwaletea maendeleo na kuweka pembeni tofauti za kisiasa.

Dk Slaa alipoulizwa jana kuhusu msimamo wa madiwani hao, alisema Katiba ya Chadema itachukua nafasi yake katika kuamua suala hilo akisema asingependa kuibua malumbano katika suala hilo wala kutunishiana misuli. Alisema diwani yoyote anayeona kwamba hakutendewa haki ana haki ya kwenda mahakamani.

"Katiba ya Chadema itakwenda kufanya kazi, kamati kuu iliwataka wajiuzulu mara moja kama wamekataa sasa katiba itachukua mkondo wake na yoyote anayeona alichafuliwa yuko tayari kwenda mahakamani," alisema.

Mgogoro huo wa umeya Arusha ulisababisha mauaji ya watu watatu katika maandamano yaliyofanyika Aprili mwaka huu, mmoja wao akiwa ni raia wa Kenya baada ya Chadema kuamua kuandamana kwa nguvu bila kibali cha polisi.

Friday, July 22, 2011

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU ZIARA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO TANZANIA JAKAYA KIKWETE SOUTH AFRIKA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Julai 20, 2011, ametumia siku ya pili ya ziara yake ya kihistoria katika Afrika Kusini kwa kutembelea na kushawishi wawekezaji wa kilimo cha zabibu na utengenezaji divai kutoka nchi hiyo kuwekeza katika kilimo cha zao hilo mkoani Dodoma.

Aidha, Rais Kikwete ametembelea Kisiwa cha Robben, kilichoko kilomita 12 kutoka mjini Cape Town ambako viongozi wakuu wa mapambano ya kupinga siasa za ubaguzi wa rangi za makaburu walifungwa kwa vipindi kirefu wakiwemo marais watatu kati ya wanne walioongozwa Afrika Kusini tokea Uchaguzi Mkuu wa Kidemokrasia wa mwaka 1994 – Waheshimiwa Nelson Mandela, Kgalema Mothlante na Jacob Zuma.

Rais mwingine ambaye ameongoza Afrika Kusini tokea wakati huo, Mheshimiwa Thabo Mbeki hakufungwa katika Kisiwa hicho lakini baba yake hayati Govin Mbeki alifungwa na akina Mandela kwenye Kisiwa hicho.

Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete na ujumbe wake ametumia siku ya pili ya ziara yake ya kidola katika Afrika Kusini kutembelea mashamba ya zabibu na kiwanda  cha kutengeneza divai katika Jimbo la Cape Magharibi ambalo mji wake mkuu ni Cape Town.

Rais Kikwete amewasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cape Town asubuhi ya leo akitokea Pretoria na kwenda moja kwa moja kutembelea Kisiwa cha Robben ambako alitembezwa kwa kiasi cha dakika 40 kabla ya kuelekea kwenye shamba na kiwanda cha kupanda zabibu na kutengeneza divai la Waterford Estate lililoko katika eneo la StellenBosch, eneo maarufu kwa zao la zabibu na utengenezaji wa divai.

Akizungumza na wenye kiwanda cha Waterford, Rais Kikwete amewaomba kufikiria kwa makini uwezekano wa kuwekeza katika mashamba ya zabibu na utengenezaji divai kwa kushirikiana na wakulima wadogo wadogo wa eneo la Dodoma.

“Naomba mfikirie kwa makini kabisa ombi langu la kuwataka mje kuwekeza katika kilimo cha zabibu na utengenezaji divai kwa kushirikiana na wakulima wa Mkoa wa Dodoma. Katika mkoa huu, zabibu huvumwa mara mbili kwa mwaka tofauti na nchi nyingine duniani na wakulima katika eneo hilo wanaweza kunufaika na ujuzi na uzoefu wenu na kuwapandia zabibu kwa ajili ya kuendesha kiwanda chenu,” Rais Kikwete amewaambia wakulima hao.

Kiwanda cha Waterford kilianzishwa Aprili mwaka 1998 na familia mbili ambazo ni ile ya Jeremy na mke wake Leigh Ord pamoja na ile ya Kevin Arnold ambaye ni mtengenezaji divai pamoja na mkewe.

Kiwanda hicho ambacho kwa sasa kinatengeneza kiasi cha masanduku 35,000 ya divai kwa mwaka ikiwa ni divai nyekundu na nyeupe ni moja ya viwanda vinavyoongoza katika Afrika Kusini kwa kutengeneza divai bora duniani.

(Att. Media: Kurugenzi ya Mawasiliano leo, Alhamisi, Julai 22, itatoa Makala Maalum kuhusu ziara ya Mheshimiwa Rais Kikwete katika Kisiwa cha Robben).


Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Pretoria
Afrika Kusini.

22 Julai, 2011
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesisitiza, kwa mara nyingine tena, kuwa Serikali yake haijapata kukusudia wala haina mipango ya kujenga barabara ya lami kukatisha katikati ya mbuga maarufu duniani ya Serengeti iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kama yupo kiongozi ambaye amethibitisha wakati wote wa uongozi wake kuwa mtetezi mkubwa wa mazingira na kulinda mbuga za wanyama basi ni yeye mwenyewe.

“Serengeti ni tunu ya taifa letu. Kamwe hatuwezi kuchukua hatua zozote za kuharibu ama hata kuvuruga hali ya Serengeti. Ni tunu ya Tanzania, ina thamani kiuchumi kwa wananchi wetu na kwa nchi yetu na ni moja ya maeneo machache duniani ambayo dunia inayatambua kwa upekee na umuhimu wake na inayalinda,” amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema hayo juzi, Jumanne, Julai 19, 2011 wakati anamjulisha Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Zuma na mawaziri wa Baraza la Mawaziri la kiongozi huyo wa Afrika Kusini kuhusu mkanganyiko ambao umezuka, kwa bahati mbaya sana duniani, kuhusu mipango ya Serikali ya Rais Kikwete kuwapatia wananchi wanaoishi Kaskazini mwa Mbuga ya Serengenti barabara ya uhakika ili kumaliza matatizo yao makubwa ya maendeleo.

Rais Kikwete alitoa maelezo hayo kwa viongozi hao wa Afrika Kusini wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Serikali za Tanzania na Afrika Kusini kwenye Majengo ya Muungano (Union Buildings) mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Mazungumzo hayo yalikuwa moja ya shughuli za mwanzo kati ya shughuli nyingi za Mheshimiwa Rais Kikwete wakati wa ziara yake ya kidola ya kihistoria ya siku tatu katika Afrika Kusini iliyomalizika jioni ya leo, Jumatano, Julai 20, 2011. Rais Kikwete anaondoka Afrika Kusini kurejea nyumbani kesho, Alhamisi, Julai 21, 2011.

Rais Kikwete alimwambia Rais Zuma na mawaziri wake kuwa umekuwepo mchanganyiko usiokuwa wa lazima kabisa kuhusu mipango ya Serikali kuwapatia barabara wananchi wa maeneo yasiyofikika kwa urahisi kati ya Mto wa Mbu, mkoani Arusha hadi Makutano, mkoani Mara kupitia Loliondo, Mugumu na Nata.

“Nataka kuzungumzia kidogo suala la madai kuwa Tanzania inataka kujenga barabara ya lami kukatisha Mbuga ya Wanyama ya Serengeti. Sijui mkanganyiko kuhusu suala hili umetoka wapi lakini ukweli ni kwamba Serikali ya Tanzania haikusudii na wala haina mipango ya kujenga barabara ya lami kupitia mbuga hii muhimu sana kwa Tanzania na kwa dunia nzima.”

“Tunachosema ni kwamba Serikali yetu inao wajibu wa aina mbili. Kwanza ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanaoishi Kaskazini mwa Serengeti wanapatiwa barabara ya uhakika ili kusaidia kufungua fursa zao za maendeleo.

 Hawawezi kuendelea kufanywa kama sehemu ya utalii kwa kubakia katika hali ya udhalili. Pili ni kuhakikisha kuwa tunalinda Mbuga la Serengeti kama ambavyo tumefanya miaka yote tokea uhuru wetu mwaka 1961.”

“ Mipango yetu ni kuhakikisha kuwa sehemu nzima ya barabara inayokatisha Mbuga hiyo inabakia bila lami na wala siyo kweli kuwa tunalenga kuharibu Mbuga hiyo. Sisi ndio watunzaji wakuu wa mbuga hii na mbuga zote za wanyama za Tanzania, inakuwaje leo sisi ndiyo tunaambiwa kuwa tunakusudia kuharibu mbuga hizo? Binafsi tokea kuchukua nafasi ya Urais wa Tanzania mapumziko yangu yamekuwa katika mbuga zetu za wanyama…hata juzi, siku nne kabla ya kuja hapa nilikuwa Serengeti.”


Aliongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Ni jambo la kusikitisha sana kuwa wapo watu ambao wanapinga ujenzi wa barabara hii ambayo wala haitakatisha kwa lami katikati ya mbuga hiyo. Wanasahau kuwa hawa watu tunaotaka kuwajengea barabara waliondolewa katika Mbuga hiyo ambamo walikuwa wanaishi. Waliondoka bila matatizo yoyote sasa kwa nini Serikali isiwajibike kwa kuwapatia nyenzo muhimu ya maendeleo kama barabara.”

Baada ya maelezo hayo, Rais Zuma alimwambia Rais Kikwete: “Tunaunga mkono moja kwa moja msimamo wa Tanzania kuhusu suala hili. Tunaelewa tatizo ambalo Serikali yako, Mheshimiwa Rais, inajaribu kulitatua la kuleta maendeleo kwa wananchi wake.”

Barabara ya Mto wa Mbu-Loliondo-Mugumu-Nata-Makutano yenye kilomita 452 ni miongoni mwa barabara zenye jumla ya kilomita 11,000 ambazo Serikali ya Rais Kikwete anazijenga ama kuanza kuzijenga katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake. Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ujenzi wa barabara hiyo unatakiwa kuanza katika kipindi cha sasa.

Akizungumza baadaye usiku katika dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais Zuma kwa ajili yake kwenye Nyumba ya Urais ya Afrika Kusini, Rais Kikwete aliisifu Serikali ya Afrika Kusini kwa kuonyesha uongozi katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili Bara la Afrika.

“Mheshimiwa Rais tulishughulikia kwa pamoja matatizo ya Burundi na sasa nchi hiyo imetulia. Umeshughulikia suala la Zimbabwe ambalo bado linahitaji jitihada zako. Kwa pamoja tulihangaika na Ivory Coast na tunawatakia heri waanze kuijenga upya nchi hiyo na sasa una changamoto ya Libya. Napenda kukupongeza kwa mchango wako katika kuleta utulivu na amani katika Bara letu.”

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Pretoria
Afrika Kusini.

22 Julai, 2011