Thursday, August 4, 2011

MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI INAZIADA YA TANI MIL 5 YA ZAO LA CHAKULA

Mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini inaziada ya tani milioni 5 za mazao ya Chakula ambazo zitasaidia kulisha mikoa mingine yenye upungufu wa Chakula.

Hayo yameelezwa na naibu waziri wa kilimo, chakula na Ushirikika Injinia Christopher Chiza wakati akifungua maonesho ya kilimo nane nane kanda ya nyanda za juu kusini ambayo yanaendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale vilivyopo kata ya Isyesye jijini Mbeya.

Amesema ziada hiyo ya chakula ni matokeo mazuri yaliyopatikana kutoka kwa wakulima baada ya Serikali kushinikiza wakulima kulima kilimo bora kwa kuzingatia kanuni za kilimo.

Aidha amewataka wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza mkoani Mbeya kwa kufungua viwanda vya usindikaji wa mazao, ambapo kupitia viwanda hivyo wakulima watanufaika kwa kiasi kikubwa katika soko la mazao yao.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile ameiomba Serikali kuwatafutia wakulima soko la ndani na nje ili waweze kunufaika kupitia kilimo.

WAMILIKI WA VITUO VYA MAFUTA JIJINI MBEYA WAGOMEA KUSHUSHA BEI


Wamiliki wa vituo vya mafuta jijini Mbeya wamegoma kushusha bei ya mafuta iliyapangwa na kutangazwa jana na mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji (EWURA.

Uchunguzi uliofanywa katika vituo kadhaa vya mafuta jijini Mbeya umebaini kuwepo kwa mgomo baridi ambapo baadhi ya vituo vimekuwa vikifungwa kwa kisingizio cha kutokuwa na mafuta.

Aidha uchunguzi huo umebaini kuwa katika maeneo mengine vituo vimekuwa vikiendelea kutoa huduma kwa bei ya zamani.

Hapo jana Serikali ilitangaza kushasha bei ya mafuta ili kuwapunguzia makali watumiaji wa badhaa hiyo nchini.

Akizungumza na wanahabari Mkurugenzi wa EWURA bwana HARUNA MASEBU amesema mafuta ya petrol yamepungua kwa shilingi 202 pointi 37 sawa na asilimia 9 nukta 17 ambapo mafuta ya dizeli yatakuwa yamepugua kwa shilingi 173 ambayo ni sawa na asilimia 8

Bwana Masebu alisema alisema bei ya mafuta ya taa imeshuka kwa shilingi 181 nukta 37 sawa na asilimia 8 nukta 70 na mabadiliko hayo yametokana na marekebisho ya yaliyofanywa na kanuni kukokotolea bei za mafuta.

hata hivyo baadhi ya wamiliki wa mafuta mkoani Mbeya wamekuwa wakiuza Petrol 2110 shilingi Dizeli 2015 shilingi na Mafuta ya taa Shilingi 2010.


HUKU NA KULE :- WANAWAKE WAJITOKEZA KUPIMA VIRUSI VYA UKIMWI
Idadi kubwa ya wanawake wamejitokeza kupima virusi vya ukimwi ndani ya viwanja vya John Mwakangale kwenye maonyesho ya nanenane jijini Mbeya yalioanza tarehe mosi Agosti mwaka huu.

Hayo yamesemwa na mmoja wa washauri wa kituo cha kupima na kutoa ushauri nasaha Kihumbe Bi.Eva Lutangilo kuwa wananchi wameonyesha mwamko mzuri kutaka kujua afya zao wakiongoza wanawake.

Ameongeza kwamba licha ya upimaji wanatoa elimu juu ya virusi ukimwi jinsi unavyoambukizwa, dalili zake na jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na ngono.

WANAFUNZI WAJISHUGHULISHA NANE NANE NYAKATI ZA MASOMO.

Baadhi ya Wanafunzi wa shule za msingi jijini Mbeya wameonekana wakijishughulisha na kazi mbalimbali katika uwanja wa maonesho ya kilimo Nane nane badala ya kuwa masomoni.

Watoto hao wamekuwa wakijishughulisha na shughuli za usafi wa mabanda, michezo ya kamali na kubeba mizigo ya baadhi ya wafanyabishara ndogondogo uwanjani humo.

Watoto hao wamekuwa wakionekana kwenye viwanja hivyo muda ambao ni wa masomo huku wakiwa wamevalia sare za shule.

Mtoto Shoham James mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Gombe iliyopo kata ya Uyole amesema ugumu wa maisha na kipato duni cha familia ndio sababu inayowafanya kushindwa kuwa masomoni muda wa masomo na badala yake wanajishughulisha na kazi mbalimbali kwenye maonesho hayo ili waweze kujipatia kipato.

Kwa Hisani ya Mtandao wa BONYEZA HAPA CHIMBUKO LETU

No comments:

Post a Comment