Sunday, July 24, 2011

Afisa ushirika jiji la Mbeya BUMI MASUBA ameusimamisha kazi uongozi wa Ilomba market Saccos kwa kipindi cha wiki 2

Afisa ushirika jiji la Mbeya BUMI MASUBA ameusimamisha kazi uongozi wa Ilomba market Saccos kwa kipindi cha wiki 2 ili kupisha uchunguzi dhidi yao wa shilingi Milioni 22 fedha ambazo zimetumika katika mazingira ya kutatanisha.

Akihitimisha mjadala uliodumu kwa zaidi ya masaa mawili Afisa ushirika aliwataka wanachama wa Ilomba Market Saccos kuchagua wajumbe watano watakao simamia uchunguzi, ambapo kamati ya Muda itakuwa na jukumu la kuwasilisha mahesabu ofisi ya halmashauri ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kwa wahusika endapo kutabainika kuwepo kwa ubadhilifu wowote wa fedha za umoja.

Walichaguliwa na wajumbe walio udhuria mkutano huo ni ALLY UHA, EVARISTO PANGANI, NDUMIGWE KAJIGIRI, BEATRICE RUASI na AGUSTINO KAPANGA.

Inadaiwa kuwa uongozi uliosimamishwa kazi chini ya Uwenyekiti wa SANGA J.SANGA ulikopa shilingi milioni 136 toka NMB na ukakopesha milioni 72 kwa wanachama wake ambapo shilingi milioni 19 zinadaiwa zimerejeshwa na shilingi milioni 31 zikiwa hazijarejeshwa hata hivyo taarifa haioneshi matumizi ya shilingi miolioni 22.

Ilomba Market Saccos inajumla ya wanachama 200 ambapo kati yao wanachama hai ni 150

Nzovwe - Jijini Mbeya.

Chuo cha maendeleo ya wananchi kilichopo kata ya Nzovwe wilaya ya Mbeya kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi hasa waalimu wa fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na masomo ya uelewa.

Akiongea katika tafrija fupi ya kuwaaga wanafunzi iliyofanyika chuoni hapo jana mkuu wa chuo hicho Bi REHEMA ASUKULYE amesema walimu waliopo ni watatu hali inayowalazimu kutafuta waalimu kutoka vyuo vingine.

Ameongeza kuwa pamoja na upungufu wa waalimu pia chuo kinadaiwa na idara ya maji shilingi milioni mbili na nusu kwa ajili ya kulipia ankra ya maji.

Kutokana na changamoto hizo ameiomba Serikali kukisaidia chuo hicho ili kiweze kukabiliana na madeni yanayowakabili.

DANNY MWAKITELEKO WA NEW HABARI COORPORATION AAGA DUNIA AACHA SIMANZI KWA WANAHABARI NCHINI TANZANIA

 NAIBU MHARIRI MTENDAJI wa Kampuni la New Habari Coorporation (2006) Limited, Danny Mwakiteleko amefariki dunia mapema leo majira ya saa 10 Alfajiri katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
 Dany Akiendelea kupata matibabu mara baada ya Kupata ajali ya Gari iliyompelekea kufanyiwa Oparesheni ya Kichwa hata Hivyo mwenyezi Mungu alimpenda zaidi na hivyo kumtwaa jana alfajiri na anatarajiwa kuzikwa Wilayani Rungwe mkoani Mbeya siku ya Juma Nne
Gari lilianzisha Safari ya Maisha mapya ya Dany Kitwana.
DANNY MWAKITELEKO HATUNAE TENA DUNIA BALI NI HISTORIA TU


ALIYEKUWA Mhariri  wa gazeti la Rai, ambaye pia ni Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari, Danny Mwakiteleko , amefariki dunia leo alfajiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na anatarajiwa kuzikwa kesho kutwa wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Mwakiteleko alilazwa katika kitengo cha watu mahtuti Muhimbili baada ya ajali aliyoipata usiku wa jumatano wiki hili eneo la Tabata na kukimbizwa katika Hospitali ya Amana, Ilala na baadaye Muhimbili.

 Katika ajali hiyo gari alilokuwa akiendesha Mwakiteleko liligongwa na lori lenye trela, ambalo lilitoweka bila kujulikana saa nne usiku. Mwakiteleko alikuwa akitokea kazini Sinza ambako alifanya kazi hadi saa tatu usiku.

Jana Rais Jakaya Kikwete alienda kumuona na kuelezwa kwamba hali yake inaendelea vyema.

Danny Mwakiteleko, amefariki dunia akiwa  na umri wa miaka 45 na anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Rugombo, Mwakaleli wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Saturday, July 23, 2011

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA MHESHIMIWA BERNAD MEMBE (MB)AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012

                                   WAZIRI MHE. BERNARD KAMILLIUS MEMBE
A. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

2. Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nachukua fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne. Pili, ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kunichagua kwa mara nyingine tena kuongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Aidha, ninampongeza Dkt. Mohammed Gharib Bilal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, ninampongeza Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, (Mb.) kwa kuchaguliwa bila kupingwa kuwa Mbunge na kuteuliwa tena na Mhe. Rais na hatimaye kuthibitishwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Waziri Mkuu kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne.

3. Mheshimiwa Spika, napenda nikupongeze kwa kuchaguliwa kwa kishindo kushika nafasi ya Spika wa Bunge letu tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu, miaka 50 iliyopita. Uteuzi wako ni kielelezo cha ukomavu wa demokrasia ya nchi yetu na imani kubwa tuliyonayo sisi Waheshimiwa Wabunge, juu ya utendaji wako uliotukuka. Kadhalika, nampongeza Naibu Spika, Mhe. Job Ndugai pamoja na Wenyeviti kwa kuchaguliwa katika kusaidia uendeshaji wa Bunge hili tukufu. Napenda pia kuwapongeza Mawaziri wenzangu pamoja na Naibu Mawaziri wote, kwa kuteuliwa kwao na Mhe. Rais kushika nyadhifa hizo. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupata heshima na dhamana kubwa ya kuwawakilisha wananchi wa majimbo pamoja na makundi mbalimbali ya jamii katika Bunge hili.
4. Mheshimiwa Spika, naomba kwa namna ya pekee niwashukuru Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) na Waziri wa Fedha, Mhe. Mustafa Haidi Mkulo (Mb.) kwa hotuba zao ambazo zimetoa mwelekeo wa Taifa letu katika mwaka huu wa fedha. Hotuba zao zimegusia mambo ya kimsingi yanayohusu Wizara yangu. Naomba pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Mawaziri wenzangu wote walionitangulia katika kuwasilisha hotuba zao kwa kuzungumzia kwa ufasaha baadhi ya masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa wanayoyashughulikia katika Wizara zao. Wizara yangu imekuwa ikishirikiana vyema na kwa karibu sana na Wizara hizi, na mara zote imekuwa ikizingatia ushauri wao kwa umakini mkubwa.

5. Mheshimiwa Spika, napenda pia niwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya Uenyekiti wa Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.) kwa ushauri wao ambao umekuwa wa msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu ya Wizara yangu kwa mafanikio.

6. Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye ameendelea kuwa wa msaada mkubwa kwangu katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Aidha, namshukuru Katibu Mkuu, Bwana John M. Haule; Naibu Katibu Mkuu, Balozi Rajabu Gamaha, Wakurugenzi wote, Mabalozi wetu pamoja na wafanyakazi wenzangu wote Wizarani na katika Balozi zetu kwa bidii na kujituma kwao ipasavyo katika kutetea na kulinda maslahi ya nchi yetu ndani na nje na pia kwa kufanikisha kwa wakati hotuba hii ya bajeti.

7. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wapiga kura wangu na wananchi wa Jimbo la Mtama, kwa upendo wao na imani yao kwangu. Napenda pia niwashukuru viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wa Mkoa wa Lindi kwa uongozi thabiti na kwa ushirikiano wao mkubwa. Kwa upande wa familia yangu, ningependa kumshukuru sana mke wangu, Dorcas Membe, pamoja na watoto wetu kwa kunitia moyo na nguvu katika shughuli zangu za kila siku. Mama Membe hayupo pale juu leo kwa sababu yupo nje ya nchi akimuuguza kijana wetu Denis ambaye amefanyiwa upasuaji mkubwa na namtakia afya njema.




B. HALI YA DUNIA NA CHANGAMOTO ZILIZOPO

8. Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi na usalama duniani kwa ujumla ni shwari isipokuwa katika maeneo machache ambayo yanahitaji uangalizi wa makini wa jumuiya ya kimataifa.

9. Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi katika nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, imeendelea kuimarika baada ya kipindi kigumu cha mdororo wa uchumi uliyoikumba dunia mwaka 2008 licha ya baadhi ya nchi kama Ugiriki, Uhispania na Ureno kuendelea kusuasua katika kuimarisha uchumi wao. Kwa ujumla, hali ya usalama duniani inatia moyo ingawa kuna maeneo machache ambayo yamegubikwa na migogoro ya ndani, iliyosababishwa na shinikizo la kutaka mabadiliko ya kisiasa, kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa ajira. Hali hiyo imeleta madhara makubwa katika nchi ambazo hazikuingia katika mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaliyoanza katika miaka ya themanini hadi miaka ya tisini. Madhara hayo ni pamoja na vifo vya raia, ongezeko la wakimbizi, uharibifu wa miundombinu, kuzorota kwa shughuli za uzalishaji na hivyo kuongezeka kwa umaskini na hatari ya kuibuka kwa vitendo vipya vya kigaidi. Wizara yangu imeendelea kufuatilia na kushiriki kikamilifu katika michakato ya kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro hiyo.

MATUKIO YA MAUAJI NA UNYANYASAJI DHIDI YA WANAWAKE SASA NI KERO MBEYA

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ADVOCATE NYOMBI akitoa taarifa ya matukio ya Ujambazi na mauaji mkoani Mbeya hapo alikuwa Mbele ya waandishi wa Habari
VITENDO HIVI VYA UNYANYASAJI WANAWAKE VISIPO CHUKULIWA HATUA ZA HARAKA TUNAHATARI YA KUSABABSHA VIFO VINGI KWA WANAWAKE NA WATOTO
MBEYA
WATU watatu wamefariki dunia mkoani Mbeya katika matukio tofauti mmoja kwa kukatwa na shoka kichwani, mwingine kwa kukatwa koromeo na kutobolewa macho huku wa tatu akiwa ameuawa kutokana na wivu wa mapenzi.

Tukio la kwanza limetokea eneo la kijiji cha Isalilo wilayani Mbozi ambapo Amina Maonezi Tuliaje (18) ambaye alikuwa Mkulima aliuawa kwa kukatwa na shoka kichwani na Nemes Muyombe ambaye ni mumewe na marehemu.

Baada ya tukio hilo shoka lililotumika katika mauaji hayo liling'ang'aniwa kichwani ambapo sababu ya mauaji hayo imeelezwa kuwa ni kupakuliwa mboga kidogo na baada ya mauaji hayo mtuhumiwa alitoroka kusikojulikana.

Tukio la pili lilitokea katika kijiji cha Isaka kata ya Nkunga wilaya ya Rungwe ambapo Alex Hezron (22) aliyekuwa mkazi wa eneo la Igogwe aliuawa kwa kukatwa koromeo lake na watu wasiofahamika ambapo mwili wake ulikutwa na majeraha mengine matatu kichwani na kisogoni.

Mwili wa marehemu huyo ulikutwa umetobolewa macho yote mawili na mwili wake ulikutwa eneo la mto Igogwe na kwamba Maerehemu alitoweka nyumbani tangu Julai 18 mwaka huu.

Katika tukio la tatu lililotokea eneo la Uturo wilaya ya Mbarali Ombeni Msigwa (31) kabila Mbena alifariki dunia akiwa anakimbizwa Hospitalini baada ya kupigwa na mumewe aitwaye Siasa Njali (32) ambapo chanzo cha mauaji hayo kimeelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi ambapo alikuwa akituhumiwa kuwa na mahusiano na wanaume wengine.

Matukio yote hayo yamethibitishwa na Kamanda wa polisiwa mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi ambaye amesema kuwa katika matukio hayo mtuhumiwa mmoja wa tukio la mauaji ya wivu wa kimapenzi amekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa na jeshi hilo.

MAANDALIZI YA SIKU YA MASHUJAA MBEYA YAENDELEA VIZURI MBEYA

 Jiwe la msingi lenye majina ya mashujaa waliokufa vitani eneo la uhindini kama linavyoonekana katika makaburi yaliyopo eneo hilo.
 Askari wa JWTZ kikosi cha 44 KJ wakiwa kwenye mazoezi ya maandalizi ya siku ya mashujaa mkoani Mbeya leo.

DK.SLAA APINGWA NA MADIWANI WAKE KUHUSU AGIZO LA KUJIHUZURU NYADHIFA ZAO

 CHADEMA YAPANGARUKA, KILA MMOJA ATAKA KUONEKANA MBABE DHIDI YA MWENZAKE:
MADIWANI watatu wa Chadema waliotakiwa kujiuzulu nyadhifa zao katika Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kufikia saa 7:02 mchana jana, wamegoma kufanya hivyo na badala yake wameutaka uongozi wa taifa wa chama hicho kuwasafisha kwa kuwataka radhi.

Kauli hiyo ya madiwani hao akiwamo Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Estomi Mallah imekuja siku chache baada ya kuvuja kwa ripoti ya kamati iliyoundwa na Chadema kuchunguza mwafaka wa madiwani wake, wa CCM na TLP katika kumpata Meya wa jiji hilo ikibainisha kuwa hakukuwa na tuhuma za rushwa katika mchakato huo.

Badala ya kujiuzulu, madiwani hao wametoa masharti magumu kwa chama hicho, licha ya kutaka kusafishwa, pia wamemtaka Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuwasafisha kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kueleza umma kwamba hawakuhongwa.

Mallah ambaye ni mwenyekiti wa madiwani hao alisema jana kuwa wamekitaka chama chao kuwaomba radhi kupitia vyombo vya habari kwa kuwa ripoti hiyo imebainisha ukweli wa mambo. Alisema taarifa za wao kuhongwa zilizotolewa na uongozi wa chama chao ziliwasababishia usumbufu mkubwa ndani ya jamii zao kiasi cha kufanya baadhi yao kunusurika kupigwa mawe.

Akizungumzia agizo la kujiuzulu nyadhifa ndani ya manispaa hadi kufikia jana saa 7:02, alisema wamepanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa kuwa hawakutendewa haki. Mallah aliutaka uongozi wa Chadema kutambua misingi ya haki huku akibanisha kuwa migogoro ya ndani kwa ndani huenda ikakipeleka mahali kubaya akisema kama kuna tatizo, linapaswa kutatuliwa kupitia vikao na si vinginevyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Elerai (Chadema), John Bayo alikwenda mbali akimtaka Lema kupita katika maeneo yote ya Jiji la Arusha kuwasafisha mbele ya wananchi kutokana na tuhuma alizozitoa kuwa walipokea rushwa.

Chadema kimetofautiana na madiwani hao kwa kile inachoeleza kuwa wamepingana na msimamo wa chama hicho kutotambua mwafaka katika mgogoro wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapinga jinsi muafaka huo ulivyofikiwa kikisema haukufuata misingi ya kisheria ba kwamba ili mwafaka upatikane mambo kadhaa yalipaswa kujadiliwa kwa pamoja ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa chama hicho kutokana na maandamano yaliyofanyika mapema mwaka huu kupinga matokeo ya uchaguzi wa meya, kulipwa fidia kwa familia za marehemu waliokufa kwenye maandamano hayo na uchaguzi wa meya wa jiji hilo kurudiwa.

Uongozi wa taifa wa chama hicho unaona kwamba kitendo cha madiwani hao kukubali nyadhifa ndani ya Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha kabla mambo hayo hayajatekelezwa, kimetafsiriwa na Kamati Kuu ya Chama hicho kuwa ni usaliti uliotokana na rushwa.

Wahudhuria kikao cha halmashauri ya jiji

Licha ya madiwani hao kupuuza agizo hilo la makao makuu ya Chadema, jana walihudhuria kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kikifanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kama kawaida huku baadhi yao wakisema sasa wameamua kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi waliowachagua ili kuwaletea maendeleo na kuweka pembeni tofauti za kisiasa.

Dk Slaa alipoulizwa jana kuhusu msimamo wa madiwani hao, alisema Katiba ya Chadema itachukua nafasi yake katika kuamua suala hilo akisema asingependa kuibua malumbano katika suala hilo wala kutunishiana misuli. Alisema diwani yoyote anayeona kwamba hakutendewa haki ana haki ya kwenda mahakamani.

"Katiba ya Chadema itakwenda kufanya kazi, kamati kuu iliwataka wajiuzulu mara moja kama wamekataa sasa katiba itachukua mkondo wake na yoyote anayeona alichafuliwa yuko tayari kwenda mahakamani," alisema.

Mgogoro huo wa umeya Arusha ulisababisha mauaji ya watu watatu katika maandamano yaliyofanyika Aprili mwaka huu, mmoja wao akiwa ni raia wa Kenya baada ya Chadema kuamua kuandamana kwa nguvu bila kibali cha polisi.

Friday, July 22, 2011

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU ZIARA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO TANZANIA JAKAYA KIKWETE SOUTH AFRIKA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Julai 20, 2011, ametumia siku ya pili ya ziara yake ya kihistoria katika Afrika Kusini kwa kutembelea na kushawishi wawekezaji wa kilimo cha zabibu na utengenezaji divai kutoka nchi hiyo kuwekeza katika kilimo cha zao hilo mkoani Dodoma.

Aidha, Rais Kikwete ametembelea Kisiwa cha Robben, kilichoko kilomita 12 kutoka mjini Cape Town ambako viongozi wakuu wa mapambano ya kupinga siasa za ubaguzi wa rangi za makaburu walifungwa kwa vipindi kirefu wakiwemo marais watatu kati ya wanne walioongozwa Afrika Kusini tokea Uchaguzi Mkuu wa Kidemokrasia wa mwaka 1994 – Waheshimiwa Nelson Mandela, Kgalema Mothlante na Jacob Zuma.

Rais mwingine ambaye ameongoza Afrika Kusini tokea wakati huo, Mheshimiwa Thabo Mbeki hakufungwa katika Kisiwa hicho lakini baba yake hayati Govin Mbeki alifungwa na akina Mandela kwenye Kisiwa hicho.

Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete na ujumbe wake ametumia siku ya pili ya ziara yake ya kidola katika Afrika Kusini kutembelea mashamba ya zabibu na kiwanda  cha kutengeneza divai katika Jimbo la Cape Magharibi ambalo mji wake mkuu ni Cape Town.

Rais Kikwete amewasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cape Town asubuhi ya leo akitokea Pretoria na kwenda moja kwa moja kutembelea Kisiwa cha Robben ambako alitembezwa kwa kiasi cha dakika 40 kabla ya kuelekea kwenye shamba na kiwanda cha kupanda zabibu na kutengeneza divai la Waterford Estate lililoko katika eneo la StellenBosch, eneo maarufu kwa zao la zabibu na utengenezaji wa divai.

Akizungumza na wenye kiwanda cha Waterford, Rais Kikwete amewaomba kufikiria kwa makini uwezekano wa kuwekeza katika mashamba ya zabibu na utengenezaji divai kwa kushirikiana na wakulima wadogo wadogo wa eneo la Dodoma.

“Naomba mfikirie kwa makini kabisa ombi langu la kuwataka mje kuwekeza katika kilimo cha zabibu na utengenezaji divai kwa kushirikiana na wakulima wa Mkoa wa Dodoma. Katika mkoa huu, zabibu huvumwa mara mbili kwa mwaka tofauti na nchi nyingine duniani na wakulima katika eneo hilo wanaweza kunufaika na ujuzi na uzoefu wenu na kuwapandia zabibu kwa ajili ya kuendesha kiwanda chenu,” Rais Kikwete amewaambia wakulima hao.

Kiwanda cha Waterford kilianzishwa Aprili mwaka 1998 na familia mbili ambazo ni ile ya Jeremy na mke wake Leigh Ord pamoja na ile ya Kevin Arnold ambaye ni mtengenezaji divai pamoja na mkewe.

Kiwanda hicho ambacho kwa sasa kinatengeneza kiasi cha masanduku 35,000 ya divai kwa mwaka ikiwa ni divai nyekundu na nyeupe ni moja ya viwanda vinavyoongoza katika Afrika Kusini kwa kutengeneza divai bora duniani.

(Att. Media: Kurugenzi ya Mawasiliano leo, Alhamisi, Julai 22, itatoa Makala Maalum kuhusu ziara ya Mheshimiwa Rais Kikwete katika Kisiwa cha Robben).


Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Pretoria
Afrika Kusini.

22 Julai, 2011
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesisitiza, kwa mara nyingine tena, kuwa Serikali yake haijapata kukusudia wala haina mipango ya kujenga barabara ya lami kukatisha katikati ya mbuga maarufu duniani ya Serengeti iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kama yupo kiongozi ambaye amethibitisha wakati wote wa uongozi wake kuwa mtetezi mkubwa wa mazingira na kulinda mbuga za wanyama basi ni yeye mwenyewe.

“Serengeti ni tunu ya taifa letu. Kamwe hatuwezi kuchukua hatua zozote za kuharibu ama hata kuvuruga hali ya Serengeti. Ni tunu ya Tanzania, ina thamani kiuchumi kwa wananchi wetu na kwa nchi yetu na ni moja ya maeneo machache duniani ambayo dunia inayatambua kwa upekee na umuhimu wake na inayalinda,” amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema hayo juzi, Jumanne, Julai 19, 2011 wakati anamjulisha Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Zuma na mawaziri wa Baraza la Mawaziri la kiongozi huyo wa Afrika Kusini kuhusu mkanganyiko ambao umezuka, kwa bahati mbaya sana duniani, kuhusu mipango ya Serikali ya Rais Kikwete kuwapatia wananchi wanaoishi Kaskazini mwa Mbuga ya Serengenti barabara ya uhakika ili kumaliza matatizo yao makubwa ya maendeleo.

Rais Kikwete alitoa maelezo hayo kwa viongozi hao wa Afrika Kusini wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Serikali za Tanzania na Afrika Kusini kwenye Majengo ya Muungano (Union Buildings) mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Mazungumzo hayo yalikuwa moja ya shughuli za mwanzo kati ya shughuli nyingi za Mheshimiwa Rais Kikwete wakati wa ziara yake ya kidola ya kihistoria ya siku tatu katika Afrika Kusini iliyomalizika jioni ya leo, Jumatano, Julai 20, 2011. Rais Kikwete anaondoka Afrika Kusini kurejea nyumbani kesho, Alhamisi, Julai 21, 2011.

Rais Kikwete alimwambia Rais Zuma na mawaziri wake kuwa umekuwepo mchanganyiko usiokuwa wa lazima kabisa kuhusu mipango ya Serikali kuwapatia barabara wananchi wa maeneo yasiyofikika kwa urahisi kati ya Mto wa Mbu, mkoani Arusha hadi Makutano, mkoani Mara kupitia Loliondo, Mugumu na Nata.

“Nataka kuzungumzia kidogo suala la madai kuwa Tanzania inataka kujenga barabara ya lami kukatisha Mbuga ya Wanyama ya Serengeti. Sijui mkanganyiko kuhusu suala hili umetoka wapi lakini ukweli ni kwamba Serikali ya Tanzania haikusudii na wala haina mipango ya kujenga barabara ya lami kupitia mbuga hii muhimu sana kwa Tanzania na kwa dunia nzima.”

“Tunachosema ni kwamba Serikali yetu inao wajibu wa aina mbili. Kwanza ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanaoishi Kaskazini mwa Serengeti wanapatiwa barabara ya uhakika ili kusaidia kufungua fursa zao za maendeleo.

 Hawawezi kuendelea kufanywa kama sehemu ya utalii kwa kubakia katika hali ya udhalili. Pili ni kuhakikisha kuwa tunalinda Mbuga la Serengeti kama ambavyo tumefanya miaka yote tokea uhuru wetu mwaka 1961.”

“ Mipango yetu ni kuhakikisha kuwa sehemu nzima ya barabara inayokatisha Mbuga hiyo inabakia bila lami na wala siyo kweli kuwa tunalenga kuharibu Mbuga hiyo. Sisi ndio watunzaji wakuu wa mbuga hii na mbuga zote za wanyama za Tanzania, inakuwaje leo sisi ndiyo tunaambiwa kuwa tunakusudia kuharibu mbuga hizo? Binafsi tokea kuchukua nafasi ya Urais wa Tanzania mapumziko yangu yamekuwa katika mbuga zetu za wanyama…hata juzi, siku nne kabla ya kuja hapa nilikuwa Serengeti.”


Aliongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Ni jambo la kusikitisha sana kuwa wapo watu ambao wanapinga ujenzi wa barabara hii ambayo wala haitakatisha kwa lami katikati ya mbuga hiyo. Wanasahau kuwa hawa watu tunaotaka kuwajengea barabara waliondolewa katika Mbuga hiyo ambamo walikuwa wanaishi. Waliondoka bila matatizo yoyote sasa kwa nini Serikali isiwajibike kwa kuwapatia nyenzo muhimu ya maendeleo kama barabara.”

Baada ya maelezo hayo, Rais Zuma alimwambia Rais Kikwete: “Tunaunga mkono moja kwa moja msimamo wa Tanzania kuhusu suala hili. Tunaelewa tatizo ambalo Serikali yako, Mheshimiwa Rais, inajaribu kulitatua la kuleta maendeleo kwa wananchi wake.”

Barabara ya Mto wa Mbu-Loliondo-Mugumu-Nata-Makutano yenye kilomita 452 ni miongoni mwa barabara zenye jumla ya kilomita 11,000 ambazo Serikali ya Rais Kikwete anazijenga ama kuanza kuzijenga katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake. Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ujenzi wa barabara hiyo unatakiwa kuanza katika kipindi cha sasa.

Akizungumza baadaye usiku katika dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais Zuma kwa ajili yake kwenye Nyumba ya Urais ya Afrika Kusini, Rais Kikwete aliisifu Serikali ya Afrika Kusini kwa kuonyesha uongozi katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili Bara la Afrika.

“Mheshimiwa Rais tulishughulikia kwa pamoja matatizo ya Burundi na sasa nchi hiyo imetulia. Umeshughulikia suala la Zimbabwe ambalo bado linahitaji jitihada zako. Kwa pamoja tulihangaika na Ivory Coast na tunawatakia heri waanze kuijenga upya nchi hiyo na sasa una changamoto ya Libya. Napenda kukupongeza kwa mchango wako katika kuleta utulivu na amani katika Bara letu.”

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Pretoria
Afrika Kusini.

22 Julai, 2011