Thursday, August 11, 2011

YALIYOJILI MKOANI MBEYA NA MBN BLOGU KATIKA KUENDELEZA TAIFA

MIUNDOMBINU MIBOVU NI CHANZO CHA KUSUASUA
Ubovu wa miundombinu ya barabara katika wilaya ya Ileje mkoani Mbeya imetanjwa ndio sababu kuu inayoleta usumbufu kusafirisha pembejeo za ruzuku ikiwemo mbolea hizo wakati wa masika

Kwa upande wake Afisa ushauri wa kilimo wilayani humo bwana Labron Kibona alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuitupia lawama wizara ya kilimo chakula na ushirika kuwa wanachelewa kutoa hela za vocha.

Wakati huo huo Wakulima wa Tarafa ya Bundali Wilayani Ileje wameilalamikia serikali kwa kitendo cha kuwacheleweshea mbolea ya ruzuku kwa madai ya kwamba wakulima hao wanategemea kilio cha mvua kitu ambacho sio cha kweli.

Akizungumza nasi mmoja wa wakulima hao kutoka kijiji cha Isongole Bwana Nickson Sengo alisema kutokana na mvua kutokuwa ya uhakika watu wengi wilayani humo wanategemea zaidi kilimo cha umwagiliaji ambacho huanza mwezi wa tisa.

Aidha Sengo anaiomba serikali kuwahisha mbolea kabla mvua hazijaanza kunyesha kufuatana na kwamba barabara nyingi katika maeneo hayo zinapitika kiangazi.

----------------
MCHUNGAJI MWALEGA AKEMEA VIKALI WIZI UNAOFANYWA NA BAADHI YA WAUMINI
Mchungaji wa KKKT Jimbo la Mbeya Dayosisi ya Konde Nazareti Mwalwega amekemea vikali wizi unaofanywa na baadhi ya waumini kwa kutomtolea MUNGU sadaka zipasazo kulingana na mapato yao.

Akihubiri katika usharika wa Iwambi ambapo Mkuu wa Jimbo la Mbeya Mchungaji Andindilile Mwakibutu akiwa katika sherehe za kumsimika Mchungaji Mmenye Mwasampeta kwa kazi za usharikani hapo amesoma kitabu cha Mithali 3:9-10 na Malaki 3:9-10 na kusisitiza kwamba kulingana na Biblia kutomtolea MUNGU sadaka ni wizi.

Mwalenga alisema kuwa kutomtolea MUNGU sadaka kama vile zaka malimbuko shukrani ni dhambi na kumtolea ni baraka kwani MUNGU humzidishia kila amtoleaye kwa moyo.

Katika kuwaandaa waumini wa usharika wa Iwambi ambao watakuwa na sikukuu ya mavuno tarehe 21 mwezi huu Mwalwega alisisitiza kila mmoja kutoa sadaka kwa moyo kulingana na uwezo wake wa hali na mali.

Pia alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waumini juu ya umuhimu wa kuwasaidia yatima wagonjwa na wenye matatizo mbalimbali bila kujali tofauli zao vilevile ibada hiyo iliyofurika watu ilipambwa na kwaya ya Jimbo kwaya kutoka usharika wa Tunduma na kwaya ya wenyeji.

-----------------
WANANCHI MKOANI MBEYA WAISHUKURU BOT.
Wakazi wa mkoa wa Mbeya wameishukuru benki kuu ya Tanzania (BOT) kwa elimu waliyoitoa juu ya kuzitambua fedha bandia.

Wakiongea nasi baadhi ya wananchi wamesema mara nyingi wamekuwa wakipokea fedha hizo pasipo wao kujua jambo ambalo linawaletea usumbufu mkubwa hasa katika maendeleo ya kiuchumi.

Naye mmoja wa wafanyabiashara wilayani Ileje Bi.Agnes Sokwa aliwaomba wananchi kuwa makini katika suala hilo na kutowafumbia macho wale wote watakaobainika kujihusisha na usambazaji wa fedha hizo.

Aidha wakazi hao wameziomba taasisi nyingine za fedha Tanzania kushirikiana na serikali katika kutoa elimu hiyo maeneo yote na muda wote ili kuhakikisha thamani ya fedha ya Tanzania inatunzwa na kuheshimiwa.

Hata hivyo hivi karibuni yalilipotiwa baadhi ya maeneo yanayoongozwa kwa upatikanaji wa pesa bandia mkoani Mbeya kuwa ni Eso, Soweto, Iyunga na Mafiati ambapo changamoto zilikuwa zikiwakabili madereva bodaboda wakati wa upokeaji wa nauli kutoka kwa abiria zao hali iliyokuwa ikichangia kupata hasara mara baada ya kurudisha chenji.

TUREJEA MSIMU WA NANENANE- WANANCHI WAPEWE ELIMU KUHUSU TTCL

Wananchi wanatakiwa kupewa elimu juu ya umuhimu wa shirika la mawasiliano Tanzania (TTCL) na huduma zake ili waweze kuzitumia kwa ufasaha.

Akizungumza mmoja wa wafanyakazi wa TTCL katika uwanja wa maonyesho nanenane jijini Mbeya bwana Amos Humbo alisema wananchi wengi wanashindwa kutumia huduma za shirika hilo kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya huduma zao.

Aliongeza kuwa huduma ya simu za mkononi haziwafikii wananchi wote kutokana na uchanga wa huduma hiyo na gharama ya minara ya mawasiliao katika shirika hilo ikizingatiwa kwamba halitegemei ruzuku kutoka serikalini.

Aidha bwana Humbo aliiomba serikali kulisaidia shirika hilo ili kuweza kufanikisha malengo yake ya kuwafikia wananchi wote na kwa gharama nafuu ili kila mwananchi aweze kunufaika na huduma hizo.



Tuesday, August 9, 2011

HUKU NA KULE MKOANI MBEYA

VIJIJI VITATU WILAYANI ILEJE VYA NUFAIKA NA HUDUMA YA MAJI MASAFI
Vijiji vitatu wilayani Ileje mkoani Mbeya vimeanza kufaidika na huduma ya maji safi yatokanayo na visima.

Hayo yamesemwa na afisa mipango wa wilaya hiyo Bwana Lawlent Swila katika mkutano wa maendeleo uliowahusisha walimu wakuu, madiwani, wanafunzi wote wa vyuo vikuu na wadau wengine wa maendeleo wilayani humo.

Amevitaja vijiji vilivyonufaika kuwa ni Isoko, Mbebe na chembe ambavyo vimejengewa visima virefu mita 90 ambapo kijiji cha Isoko kimefungwa bomba za kupitisha maji safi.

Naye diwani wa kata ya Bupigu Ubatizo Songa ametoa pongezi kwa Serikali wilayani humo katika kuwafikishia wananchi wake huduma muhimu ya maji na kuwataka viongozi wenzake kushirikiana kikamilifu kuilinda miradi hiyo isiharibiwe.

CHUO KIKUU CHA KILIMO SOKOINE KIMETOA ELIMU KWA JAMII UMUHIMU WA CHAKULA

Chuo kikuu cha kilimo Sokoine kimetoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chakula kwa binadamu katika maadhimisho ya maonesho ya kilimo nane nane mkoani Mbeya.

Mkuu wa chuo hicho profesa Joyce Kinabo amesema jamii inatakiwa kujua umuhimu wa vyakula mbalimbali katika kujenga miili yao.

Wakati huohuo ameitaka jamii kunywa maji mara pamoja na matunda kwani kwa kufanya hivyo kutasawasaidia kujenga afya zao.


WAZIRI DAVID MATAHAYO ATOA PONGEZI KWA MKUU WA MKOA WA MBEYA BWANA MWAKIPESILE
Waziri wa mifugo na Biashara David Mathayo ametoa pongezi kwa mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakangale kwa juhudi alizozionesha kutokomeza ugonjwa wa mafua ya Nguruwe.

Amesema hayo wakati akifunga maonesho ya kilimo nane nane Ambayo yamefanyika kikanda mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale vilivyopo kata ya Uyole jijini hapa.

Aidha ametoa pongezi kwa viongozi wa mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini kwa kusimamia na kutekeleza vyema Sera ya kilimo kwanza kwa kufanikiwa kuzalisha mazao mengi ambapo mikoa hiyo Mbeya, Iringa Rukwa na Ruvuma imefanikiwa kuzalisha zaidi ya Tani milioni 5 za chakula kwa msimu huu wa kilimo ambazo zitasaidia kupunguza tatizo la njaa hapa nchini.

Wakati huohuo Waziri Mathayo amemtunuku mshindi wa kanda katika maonesho hayo Dickson Sengo mkulima wa kata ya Isongole wilayani Ileje mkoani Mbeya power Tiller moja na Cheti cha Ushindi.

Kwa hisani ya CHIMBUKO LETU 

Saturday, August 6, 2011

SHILINGI MIL 52 ZIMETOLEWA KUTUMIKA KIPINDI CHOTE CHA MAONESHO YA NANENANE MKOANI MBEYA

Zaidi ya shilingi milioni 52 zimetolewa kutumika katika kipindi chote cha maonesho ya kilimo Nanenane yanayoendelea kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile amesema fedha hizo ni kwaajili ya shughuli za maonesho ili yafanywe na ya vutie miongoni mwajamii.

Aidha ameitaka kamati ya kusimamia maonyesho hayo kuakikisha fedha zilizopatikana zinatumika kama ilivyo kusudiwa na kuwataka wamiliki wa wa vibanda vilivyopo nje ya uwanja huo kuvikamilisha ili kuondokana na hatari ya kufutiwa usajili wa maeneo yao.
HABARI ZA HUKU NA KULE.
WALEMAVU WAVVU NCHINI TANZANIA WASHAURIWA WASIKATE TAMAA

Watu wenye ulemavu na wale wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi wameshauriwa kutokata tamaa ya maisha pindi wanapakabiliana na changamtoto mbalimbali ndani ya jamii.

Ushauri huo umetolewa na mkuu wa kikundi cha jipe moyo bwana Kaspery Ngairo wakati wa mahojiano kuhusu mpango walionao kuwawezesha watu wenye ulemavu na wale wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi

Amesema watu wenye ulemavu wanamchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza shughuli za kimaendelea hapa nchini nakwamba jamii inatakiwa kuondokana na dhana ya kuwa walemavu hawana mchango katika kukuza na kuleta maendeleo ya Taifa.

Aidha Ngairo ameiomba jamii kuondokana na dhana ya kuwa ukimwi una ambukizwa kwa kula ama kuzungumza na mtu mwenye maambukizi hayo na badala yake amewataka kutambua kuwa mtu unaweza kupata maambukizi ya Virusi vya ukimwi kwa kuchangia nyembe, Ngono zembe, kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na Uchangiaji wa damu isiyo salama.

WILAYA YA KILOLO MKOANI IRINGA YAONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO MWAKA HUU.


Halmashauri ya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa imeongeza uzalishaji wa mazao mwaka huu kutokana na wakulima kutumia mbegu bora pamoja na kilimo cha umwagiliaji.

Hayo yamesemwa na Afisa kilimo wa wilaya hiyo Bwana Logan Moses katika maonesho ya kilimo Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Amesema kuwa zao la mahindi limepanda kutoka tani elfu 82 hadi kufikia tani elfu 91 na vitunguu kutoka tani elfu 80 hadi kufikia tani laki moja huku nyanya imepanda kutoka tani laki moja na thelathini na moja hadi kufikia tani laki moja na sitini na tano.

Aidha amewataka wananchi hususani vijana kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuongeza nguvu katika kilimo ili kuleta maendeleo kwa jamii na taifa kwa ujumla.

 BEI YA MAHINDI YASHUKA KWA ASILIMIA 3 WILAYANI MOMBA MKOANI MBEYA.
Bei ya gunia la mahindi imeshuka kutoka shilingi elfu 31 hadi kufikia elfu 28 wakati debe la maharage kushuka kutoka elfu 22 hadi shilingi elfu 18 katika wilaya ya Momba mkoani Mbeya.

Wafanyabiashara na wakulima wa wilayani hiyo wamesema kushuka kwa bei ya mazao kunatokana na kuwepo kwa mavuno mengi .

Mmoja wa wakulima hao Bwana Elius Kaminyoge amesema pamoja na kushuka kwa mahindi na maharage katika soko la majengo pia zao la ulezi limeshuka kutoka shilingio elfu 43 hadi kufikia shilingi elfu 41 kwa gunia na vitunguu kushuka toka shilingi elfu 25 hadi kufikia elfu 18 kwa debe.

Amesema sababu ya kushuka kwa bei ya mazao hayo kunatokana na wakulima kuingiza mazao kwa wingi sokoni hapo.

Kwa hisani ya  CHIMBUKO LETU

Thursday, August 4, 2011

MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI INAZIADA YA TANI MIL 5 YA ZAO LA CHAKULA

Mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini inaziada ya tani milioni 5 za mazao ya Chakula ambazo zitasaidia kulisha mikoa mingine yenye upungufu wa Chakula.

Hayo yameelezwa na naibu waziri wa kilimo, chakula na Ushirikika Injinia Christopher Chiza wakati akifungua maonesho ya kilimo nane nane kanda ya nyanda za juu kusini ambayo yanaendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale vilivyopo kata ya Isyesye jijini Mbeya.

Amesema ziada hiyo ya chakula ni matokeo mazuri yaliyopatikana kutoka kwa wakulima baada ya Serikali kushinikiza wakulima kulima kilimo bora kwa kuzingatia kanuni za kilimo.

Aidha amewataka wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza mkoani Mbeya kwa kufungua viwanda vya usindikaji wa mazao, ambapo kupitia viwanda hivyo wakulima watanufaika kwa kiasi kikubwa katika soko la mazao yao.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile ameiomba Serikali kuwatafutia wakulima soko la ndani na nje ili waweze kunufaika kupitia kilimo.

WAMILIKI WA VITUO VYA MAFUTA JIJINI MBEYA WAGOMEA KUSHUSHA BEI


Wamiliki wa vituo vya mafuta jijini Mbeya wamegoma kushusha bei ya mafuta iliyapangwa na kutangazwa jana na mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji (EWURA.

Uchunguzi uliofanywa katika vituo kadhaa vya mafuta jijini Mbeya umebaini kuwepo kwa mgomo baridi ambapo baadhi ya vituo vimekuwa vikifungwa kwa kisingizio cha kutokuwa na mafuta.

Aidha uchunguzi huo umebaini kuwa katika maeneo mengine vituo vimekuwa vikiendelea kutoa huduma kwa bei ya zamani.

Hapo jana Serikali ilitangaza kushasha bei ya mafuta ili kuwapunguzia makali watumiaji wa badhaa hiyo nchini.

Akizungumza na wanahabari Mkurugenzi wa EWURA bwana HARUNA MASEBU amesema mafuta ya petrol yamepungua kwa shilingi 202 pointi 37 sawa na asilimia 9 nukta 17 ambapo mafuta ya dizeli yatakuwa yamepugua kwa shilingi 173 ambayo ni sawa na asilimia 8

Bwana Masebu alisema alisema bei ya mafuta ya taa imeshuka kwa shilingi 181 nukta 37 sawa na asilimia 8 nukta 70 na mabadiliko hayo yametokana na marekebisho ya yaliyofanywa na kanuni kukokotolea bei za mafuta.

hata hivyo baadhi ya wamiliki wa mafuta mkoani Mbeya wamekuwa wakiuza Petrol 2110 shilingi Dizeli 2015 shilingi na Mafuta ya taa Shilingi 2010.


HUKU NA KULE :- WANAWAKE WAJITOKEZA KUPIMA VIRUSI VYA UKIMWI
Idadi kubwa ya wanawake wamejitokeza kupima virusi vya ukimwi ndani ya viwanja vya John Mwakangale kwenye maonyesho ya nanenane jijini Mbeya yalioanza tarehe mosi Agosti mwaka huu.

Hayo yamesemwa na mmoja wa washauri wa kituo cha kupima na kutoa ushauri nasaha Kihumbe Bi.Eva Lutangilo kuwa wananchi wameonyesha mwamko mzuri kutaka kujua afya zao wakiongoza wanawake.

Ameongeza kwamba licha ya upimaji wanatoa elimu juu ya virusi ukimwi jinsi unavyoambukizwa, dalili zake na jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na ngono.

WANAFUNZI WAJISHUGHULISHA NANE NANE NYAKATI ZA MASOMO.

Baadhi ya Wanafunzi wa shule za msingi jijini Mbeya wameonekana wakijishughulisha na kazi mbalimbali katika uwanja wa maonesho ya kilimo Nane nane badala ya kuwa masomoni.

Watoto hao wamekuwa wakijishughulisha na shughuli za usafi wa mabanda, michezo ya kamali na kubeba mizigo ya baadhi ya wafanyabishara ndogondogo uwanjani humo.

Watoto hao wamekuwa wakionekana kwenye viwanja hivyo muda ambao ni wa masomo huku wakiwa wamevalia sare za shule.

Mtoto Shoham James mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Gombe iliyopo kata ya Uyole amesema ugumu wa maisha na kipato duni cha familia ndio sababu inayowafanya kushindwa kuwa masomoni muda wa masomo na badala yake wanajishughulisha na kazi mbalimbali kwenye maonesho hayo ili waweze kujipatia kipato.

Kwa Hisani ya Mtandao wa BONYEZA HAPA CHIMBUKO LETU

Tuesday, August 2, 2011

MIAKA 50 YA UHURU MKOA WA MBEYA TUMESONGA MBELE

 TUMETOKA MBALI KITUO CHA MABASI MBEYA MIAKA YA 1970,Ktiuo cha mabasi yaendayo mikoani uhindini mbeya enzi hizo za miaka ya 70

                                                 MBEYA IRINGA MIAKA YA 1960
 Hapa ni usangu barabara ya mbeya iringa miaka ya 60,Barabara ilikuwa haina Rami matope kwa sana na ulikuwa na uwezo wa kusafiri Mbeya Iringa kwa zaidi ya siku 2

KWA PICHA HII YA CHINI VIONGOZI WA HALMASHAURI MKOA WAPI KUSIMAMIA SHERIA MLIZOZIWEKA WENYEWE?
Hapa ni uzio wa soko la mwanjelwa linalojengwa wafanya biashara hawalioni tangazo hilo?Hili ni eneo la Mwanjelwa na huo ni uzio uliowekwa wakati ujenzi wa soko la Mwanjelwa ukiendelea.

Sunday, July 31, 2011

MBUNGE WA ILEJE APANIA KUKUZA KIWANGO CHA ELIMU JIOMBINI KWAKE


MBUNGE WA ILEJE ATOA VITAMBU 1000 KUENDELEZA ELIMU JIMBONI KWAKE
Mbunge wa jimbo la Ileje mkoani Mbeya kupitia Chama Cha Mapinduzi ALIKO KIBONA ametoa vitabu elfu moja kwa shule za Sekondari wilayani humo ikiwa ni moja ya ahadi zake katika kuendeleza elimu jimboni kwake.

Akitoa msaada huo mheshimiwa Mbunge KIBONA amesema msaada huo umelenga kupunguza tatizo la vitabu mashuleni ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanafunzi kuwa na uwezo wa kusoma vitabu kwa usía.

Afisa elimu wa wilaya ya Ileje MAY KITIMA ametoa pongezi kwa mbunge huyo kwa kuchangia vitabu elfu moja vitakavyo gawiwa kwa shule 18 za Sekondari ambapo kila shule itapata mgao wa vitabu 50.

Nao madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ileje wameahidi kutoa ushirikiano na mbunge wao kwa kuhimiza wananchi kuchangia shughuli mbalimbali za kimaendeleo hasa katika elimu.

RUVUMA WAJIHIMARISHA KATIKA MAONESHO YA NANE NANE YA KANDA

Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Mkoani Ruvuma imeweka mikakati ya kuwawezesha wakulima kwa kuwapa elimu kuhusiana na kilimo  na ufugaji bora wa wanyama mbalimbali katika maonyesho ya kilimo nyanda za juu kusini kwenye viwanja vya John Mwakangala vilivyopo kata ya Isyesye.

Hayo yamesemwa na bwana GISLA MBUNGU mmoja ya wakulima walio nufaika na mafunzo ya kilimo kutoka wilayani Mbinga katika kijiji cha Mtama.

Bwana Mbungu amesema kuwa mwaka huu wakulima wataelimishwa kuhusiana na uhifadhi wa mazingira katika shughuli zao za kilimo ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo ni changamoto kubwa kwa maendeleo ya kilimo hapa nchini.

Naye ELISI MATESO kutoka kampuni ya DAE LIMITEDI inayojihusisha na uzalishaji wa kahawa wilayani Mbinga amesema kuwa wakulima watapewa mafunzo ya utunzaji miche ya kahawa, usindikaji na matumizi ya zao hilo.

Maonesho ya kilimo nane nane yanaanza kesho katika vinwanja vya JOHN MWAKANGALE

OFISI YA USTAWI WA JAMII YATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUFUATA MISINGI YA SHERIA

SERIKALI imewataka maafisa ustawi wa jamii kubuni miradi mbalimbali itakayoweza kuwasaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kujikwamua katika janga la umaskini.

Hayo yamesemwa jana na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya Moses Chitama wakati akifungua mkutano wa ufunguzi tawi la chama cha Ustawi wa Jamii (Taswa).

Amesema Maafisa wa Ustawi wa Jamii wanatakiwa kuwa chachu ya maendeleo katika jamii inayowazunguka kwa kuwa wabunifu wa miradi ya maendeleo na kufanya kazi kwa moyo moja wa kusaidia watu waishio katika mazingira magumu.

Ameongeza kuwa zimeibuka asasi ambazo zinaangalia maslahi yao wakati wanapewa fedha nyingi na wafadhili kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye matatizo ndani ya jamii.

Amesema ili kuondokana na jamii yenye vijana wanaioshi katika mazingira hatarishi, ofisi ya ustawi wa jamii inatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya utawala na kanuni za kazi zao.

BURIANI MSTAHIKI MEYA WA RUVUMA

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Ali Saidi Manya, Diwani wa kata ya Lizaboni(Mwenye suti Nyeupe) amefariki dunia leo katika Hospitali ya Misheni Peramiho.

Taarifa za Msiba huo zimetangazwa na naibu Meya wa Manispaa ya Songea Mheshimiwa Mariam Dizumba na kupokelewa kwa mshtuko mkubwa na wakazi wa manispaa ya Songea Mkoa wa ruvuma kwa ujumla.

Naibu Meya Dizumba amesema mazishi ya Mstahiki Meya Ali Saidi Manya yatafanywa nyumbani kwake Lizaboni Manispaa ya Songea Siku ya Jumatatu Tarehe 1 Agosti 2011. Maandalizi yanaendelea na wageni kadhaa wa vyeo mbalimbali wamethibitisha kuhudhuria.